Na Mary Mwakapenda- Dodoma
Naibu Waziri, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Mhe. Deogratius Ndejembi amewataka Maafisa Utumishi katika taasisi za umma nchini kuwajibika ipasavyo, kushughulikia na kutoa ufafanuzi wa masuala ya kiutumishi katika maeneo yao ya kazi kwa kuzingatia Sheria, Kanuni na Taratibu badala ya kukiuka au kuwashauri waajiri wao vibaya na kutaka Katibu Mkuu Utumishi kufanya kazi kwa niaba yao.

Mhe. Ndejembi ametoa maelekezo hayo leo Jijini Dodoma wakati akifungua kikao kazi cha siku mbili kwa Wanasheria na Maafisa Utumishi kutoka Halmashauri 31 nchini chenye lengo la kutambua changamoto zinazojitokeza katika utekelezaji wa Sheria ya Utumishi Wa Umma Sura 298 ili kuzitafutia ufumbuzi na kuboresha utoaji wa huduma kwa Watumishi wa Umma.

Mhe. Ndejembi amesema barua nyingi za kuomba ufafanuzi wa masuala mbalimbali ya kiutumishi zinazojibiwa na Ofisi yake zinaonesha Maafisa Utumishi hawawajibiki ipasavyo kwa kuwa Sheria, Kanuni, Taratibu na Nyaraka mbalimbali zipo lakini hawazitumii, badala yake Wakuu wa Taasisi wanapitisha au kuandika barua Utumishi ili Katibu Mkuu Utumishi azifanye kwa niaba yao.

“Kumbukeni ‘upward delegation is insubordination’ huu ni ukiukaji mkubwa wa sheria na ni utovu wa nidhamu ambao hauvumiliki. Hatutasita kumchukulia hatua Kiongozi yeyote atakayemtaka Katibu Mkuu Utumishi kufanya majukumu yake.” Mhe. Ndejembi amesisitiza.

Mhe. Ndejembi amewataka Maafisa Utumishi hao kujitafakari kabla ya kuomba kupewa miongozo juu ya masuala ambayo yako ndani ya mamlaka yao kwa mujibu wa Sheria, la sivyo watakuwa wanatenda makosa ambayo yanaweza kumaanisha kutotii au kuonekana wanatekeleza majukumu yao chini ya viwango.

Ametolea mfano Sheria ya Utumishi wa Umma, Sura ya 298, Kanuni za Kudumu katika Utumishi wa Umma za Mwaka 2009 pamoja na Nyaraka mbalimbali zimeainisha bayana taratibu zinazopaswa kufuatwa katika kushughulikia masuala mbalimbali ambayo ni pamoja na utaratibu wa kuwasilisha mapendekezo ya upekuzi, likizo bila malipo, Ajira za Mikataba, Upandishwaji vyeo kwa utaratibu wa kawaida na mserereko, uhamisho na ubadilishaji kada watumishi.

“Badala ya Maafisa husika kuwashauri wakuu wa Taasisi zao kwa kuzingatia miongozo iliyopo wanawashauri vibaya viongozi wao kuandika barua utumishi kuomba maelekezo na ufafanuzi.” Mhe. Ndejembi ameongeza.

Mhe. Ndejembi amesema wakati mwingine waajiri wanawasilisha mapendekezo ya kukaimu nafasi za uongozi kwa Maafisa ambao hawana sifa, na kuongeza kuwa hali hii inatoa tafsiri mbili kuwa Wakuu wa Idara za Utawala na Utumishi wanawashauri vibaya Wakuu wa Taasisi ama kwa makusudi au kwa kutowajibika kusoma Miongozo husika.

Amesema baadhi wanawapandisha vyeo watumishi wakati hawana sifa zilizoainishwa katika Miundo ya Utumishi, hali inayowaathiri watumishi husika kwa sababu maombi ya kubadilisha mishahara ili ilingane na vyeo vipya yasipoidhinishwa na Ofisi yake, huwashusha ari na morali ya kazi na hivyo kuongeza malalamiko na manungúniko.

Akitoa maelezo ya awali kuhusu kikao kazi hicho, Naibu Katibu Mkuu, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Dkt. Francis Michael amesema masuala ya kusimamia utumishi ni magumu sana, hivyo ili kuifanya kazi iwe rahisi ni jukumu la Maafisa Utumishi kujua kwa usahihi Sheria, Kanuni, Taratibu na Miongozi ili kupunguza malalamiko na kutoiingizia Serikali hasara kutokana na maamuzi mengi ya kinidhamu yanayofanywa kimakosa.