JUMA MWAMBUSI ameomba kukaa kando kwa sasa ndani ya kikosi cha Yanga kwenye majukumu ya kuwa kocha msaidizi.

Hatua hiyo imefikia baada ya yeye mwenyewe kuandika barua baada ya kikosi hicho kutwaa taji la Mapinduzi ambapo iliifunga Simba kwa penalti 4-3 baada ya dakika 90 kukamilika kwa sare ya bila kufungana, Uwanja wa Amaan, Visiwani Zanzibar.

Kwa mujibu wa Mwenyekiti wa Klabu ya Yanga, Mshindo Msolla,  kwenye barua yake ya kuomba kujiweka kando, ametaja sababu kuwa ni kuwa na matatizo ya kiafya.

Ameongeza kuwa ameshauriwa na wataalamu kukaa sehemu ambayo itamfanya asiwe na msongo wa mawazo pamoja na pasiwe na kelele.

Kwa sasa timu itakuwa chini ya Kocha Mkuu, Cedric Kaze, raia wa Burundi ambaye ameachiwa jukumu la kusaka msaidizi wake.