WAKATI Kocha Mkuu wa Yanga, Cedric Kaze, akisema kukosekana kwa kiungo, Clatous Chama na Luis Miquissione kulisaidia timu yake kutwaa ubingwa wa mashindano ya Kombe la Mapinduzi, Kaimu Kocha Mkuu wa Simba, Selemani Matola amesema uchovu waliokuwa nao wachezaji wake uliwanyima ushindi.

Yanga ilitwaa ubingwa wa mashindano hayo kwa mwaka huu kwa penalti 4-3, baada ya kutoka suluhu katika dakika 90 za kawaida kwenye mchezo huo wa fainali uliochezwa juzi usiku.

Akizungumza na gazeti hili baada ya fainali hiyo, Kaze alisema mchezo huo ulikuwa mzuri na wenye ushindani mkubwa kwa wakati wote.


Kaze alisema wachezaji wake walicheza kiufundi na kimbinu zaidi katika dakika zote 90 na anaamini kutokuwapo kwa Chama na Miquissione imewasaidia kutwaa ubingwa wa michuano hiyo.


Kocha huyo alisema kutokuwapo kwa nyota kuliwasaidia 'kuishika' Simba katika eneo la kiungo na pembeni kutowapa nafasi ya kupeleka mipira kwa washambuliaji wa mabingwa hao watetezi wa Ligi Kuu Tanzania Bara.


"Nyota hao wawili ni hatari sana wakiwapo katika kikosi, lakini niliwaambia wachezaji wangu kutoruhusu Simba kupiga krosi." Kwa sababu kama wangeruhusu kupiga krosi na ingemfikia, Meddie Kagere nina imani ingekuwa hatari, maana ninavyomjua ni hatari kwa mipira ya vichwa," alisema Kaze.

Alisema pia kombe walilolipata ni zawadi kwa wanachama na mashabiki wa Yanga ambao kwa muda mrefu hawajachukua kombe lolote, hivyo ni haki yao washangilie.

"Wana-Yanga wamebezwa sana na wamekuwa wanyonge kwa muda mrefu. Hawajachukua kombe lolote kwa muda sasa, kwa hiyo hili kombe ni lao na wanastahili kushangilia," Kaze alisema.

Kocha huyo raia wa Burundi alisema kwa sasa anaitengeneza timu yake iwe na ari ya ushindi, na iwe inacheza mechi bila kujali mazingira yoyote.

"Nataka tucheze bila kisingizio cha mvua, jua, uwanja mbovu, sijui nini. Nataka niwe na kikosi ambacho hakitokuwa na kisingizio, tukifungwa basi tunajua ni sababu ya kiufundi," alisema Kaze.

Naye Matola alisema mechi walizocheza mfululizo wachezaji wake zimewaathiri na baadhi yao kulazimika kuwatumia katika mchezo huo wa fainali huku wakiwa majeruhi.

"Tunawapongeza Yanga, wametwaa ubingwa kwa kutufunga kwa penalti, mfululizo wa mechi umetuathiri maana wachezaji wangu ikiwamo Hassan Dilunga na Miraji Athuman wakilalamika maumivu, fatiki waliyokuwa nayo imechangia kutochukuwa ubingwa," alisema Matola.

Aliongeza baada ya matokeo hayo wanarejea nyumbani na kupumzika kwa muda wa siku saba na baadaye watarejea kwa ajili ya maandalizi ya mechi za Ligi Kuu Bara na za michuano ya Ligi ya Mabingwa Afrika hatua ya makundi itakayoanza mwezi ujao.

Hata hivyo, Matola alisema waamuzi wa mechi hiyo walishindwa kuumudu mchezo huo kwa kuacha kutoa uamuzi pale nyota wake wanapofanyiwa madhambi na wachezaji wa Yanga.

Simba na Yanga tayari zimesharejea jijini Dar es Salaam, lakini Azam FC yenyewe imebakia Zanzibar kwa ajili ya kuweka kambi ili kujiimarisha na hatua ya lala salama ya Ligi Kuu Tanzania Bara ambayo itaanza tena mapema mwezi ujao.