WATUMISHI watano wa Hospitali ya Wilaya ya Nansio Ukerewe wamesimamishwa kazi kupisha uchunguzi wa vyombo vya maadili ya utumishi wa umma pamoja na maadili ya mabaraza na bodi za kitaaluma.

 

Watumishi hawa ni wale sita waliokuwa wamefikishwa mahakamani kujibu tuhuma za wizi wa dawa zenye thamani zaidi ya shilingi Milioni 200 ambapo mmoja wao alikiri na kuhukumiwa kulipa milioni 100 na waliobakia walirejeshwa kazini.

 

Watumishi hao wamesimamishwa kazi kufuatia agizo la Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto, Dkt. Dorothy Gwajima, alipofanya ziara katika Hospitali hiyo hivi karibuni ambapo, alielezwa na Mkuu wa Wilaya ya Ukerewe, Cornel Magembe, kuwa naye hakuridhishwa na watumishi hao kurejeshwa kazini kwani hawaaminiki tena kwenye utumishi wa umma na kamwe haiwezekani NA haieleweki inawezekanaje mtumishi wa umma aibe halafu akishalipa anarejeshwa kazini.

 

baada ya Gwajima kutembelea Hospitali ya Halmashauri ya Nansio alijionea kuendelea kuwepo kwa viashiria vya udanganyifu katika mfumo mzima wa ugavi wa dawa, hivyo kukubaliana na maelezo ya Mkuu wa Wilaya kuwa bado kuna tatizo kama alivyoeleza.

 

Hivyo, alimuagiza Mkurugenzi wa Wilaya ya Ukerewe, Bi. Esther Chaula, kuwasimamisha kazi watumishi hao na kuwafikisha kwenye kamati ya maadili ya utumishi wa umma, mabaraza na bodi za kitaaluma na vyama vyao ili waone kama kweli hao watumishi bado wanastahili kuaminika tena kwa mujibu wa sheria za utumishi wa umma.

 

“Mahakama imefanya maamuzi kwa mujibu wa sheria wakalipa, hata hivyo naagiza Mkurugenzi kama tulivyokubaliana uendelee kusimamia hatua za kinidhamu na kiutumishi pia uwafikishe kwenye mabaraza na bodi zao za taaluma pamoja na vyama vyao vya taaluma ili nao wawachunguze na kuwachukulia hatua,” alisema Gwajima.

 

Kwa mujibu wa Mganga Mkuu wa Mkoa wa Mwanza, Dkt. Thomas Rutachunzibwa,  watumishi hao ambao ni wataalamu wa maabara, famasi na daktari, wameshasimamishwa kazi