Kamilisheni nyumba za walimu wangu mapema- Waziri Jafo
Na Atley Kuni- KAGERA
Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa Mhe. Selemani Jafo, amewataka wajenzi wa nyumba za walimu katika Shule ya Sekondari Rugambwa kukamilisha ujenzi wa Nyumba hizo za walimu unaoendelea hivi sasa ili pindi shule zitakapofunguliwa walimu hao wawe katika Mazingira bora yakuishi.
Waziri Jafo amefikia adhma hiyo muda mfupi baada yakutembelea na kugagua ujenzi wa nyumba za walimu sita unaoendelea kujengwa katika shule hiyo ambapo tarehe na muda uliokuwa umewekwa kuhusiana na ukamilishaji nyumba hizo umekwisha toka Oktoba, 2020.
“Ndugu zangu natambua kulikuwepo na changamoto ya Saruji katika kipindi cha nyuma, lakini hiyo isiwe sababu yakutukwamisha kukamilisha ujenzi huu kwa wakati, alisema Waziri Jafo, na kuongeza kuwa, “Nilitegemea kuona kazi hapa zinakwenda sambamba kulingana na asili ya ujenzi wenyewe, mathalani, wakati mafundi wengine wanaweka vigae basi wengine wanaendelea na uwekaji wa madirisha nk.
Awali akisoma taarifa ya Ujenzi huo, Mkuu wa Shule ya Sekondari Rugambwa Kagemulo Lupaka, alisema, walipokea fedha kiasi cha shilingi za kitanzania. Milioni 701,857.003 tarehe 25 Juni, 2020 kutoka Wizara ya Elimu, sayansi na Teknolojia kwa ajili ya ujenzi nyumba sita za walimu, na ujenzi ilipaswa mapema mwezi Oktoba,2020, lakini kutokana na changamoto ya ukosefu wa Saruji katika Manispaa ya Bukoba, ukosefu wa mafofali yenye viwango stahiki na kupanda ghafla kwa bei ya saruji, bati na nondo, kulisababisha kuchelewa kwa ujenzi.
Taarifa hiyo ya Mkuu wa Shule, inaonesha kuwa nyumba nne kati ya sita zipo katika hatua ya ukamilishaji na zitakabidhiwa tarehe 22 Januari, 2021, aidha nyumba moja ipo katika hatua ya kuezekwa ilihali nyumba moja ya mwisho ipo katika hatua ya msingi.
“Mhe. Waziri mradi wa nyumba sita kwa ajili ya familia tisa, katika shule ya Sekondari Rugwambwa tunakuahidi kuwa utakamilika ifikapo Februari 25,2021” ambapo Nyumba zote sita zitakuwa zimekabidhiwa kwa wahusika amesema Lupaka.
Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais-TAMISEMI, yupo katika Mikoa ya Kanda ya Ziwa kukagua shughuli mbali mbali za maendeleo, ambapo akiwa katika Manispaa ya Bukoba na Halmashauri ya Wilaya ya Bukoba, alikagua ujenzi wa bweni kwenye Shule ya Sekondari Bukoba, ujenzi wa nyumba sita za walimu katika Shule ya Sekondari Rugambwa pamoja na Hospitali ya Wilaya ya Bukoba, ambapo sehemu zote ameonesha kuridhishwa na hali ya miradi hiyo na kuwataka waitunze idumu kwa kipindi kirefu.