Kaimu Mkurugenzi Atumbuliwa kwa Kusafirisha Maiti Juu ya Carrier ya Gari.


WAZIRI wa Nchi Ofisi ya Rais Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (TAMISEMI) Selemani Jafo amemuagiza Katibu Mkuu wa Ofisi hiyo Mhandisi Joseph Nyamuhanga kumsimamisha kazi Kaimu Mkurugenzi wa halmashauri ya Mji wa Tarime mkoani Mara Jumanne Yassin ili kupisha uchunguzi, kufuatia kitendo cha halmashauri hiyo kusafirisha mwili wa Mkuu wa Idara ya Maendeleo ya Jamii Emmanuel Sizo juu ya Carrier ya gari


Waziri Jafo ametoa agizo hilo baada ya gari iliyobeba mwili wa Mtumishi huyo kusambazwa katika mitandao mbalimbali ya kijamii.

Amesema amesikitishwa na kitendo hicho ambacho ni kinyume na kanuni za utumishi wa Umma, pamoja na mila na desturi za Mtanzania.

 Ameagiza Watumishi wote waliohusika na uzembe huo wachukuliwe hatua za kinidhamu kwa mujibu wa sheria, kanuni na taratibu za utumishi wa Umma.

Emmanuel alifariki Januari 10, 2021 katika ajali ya gari iliyotokea mkoani Singida.