Wanajeshi wa Uganda wanaohudumu kama sehemu ya jeshi la kulinda amani nchini Somalia wamewauwa wapiganaji 189 wa kundi la al-Shabaab lenye mafungamano na mtandao wa kigaidi wa al-Qaeda baada ya kuishambulia moja ya kambi zao. 

Taarifa ya Jeshi la Ulinzi la Uganda - UPDF imesema wanajeshi wake jana waliyavamia maficho ya al-Shabaab katika vijiji vya Sigaale, Adimole na Kayitoy, kusini magharibi mwa mji mkuu Mogadishu. 

Waliwauwa wapiganaji hao na kuharibu nyezo za kijeshi na vifaa vinavyotumiwa katika mashambulizi ya kigaidi. 

Hakujawa na kauli yoyote kutoka kwa al-Shabaab kuhusu shambulizi hilo. 

Wanajeshi wa Uganda ni sehemu ya ujumbe wa kulinda amani wa Umoja wa Afrika nchini Somalia - AMISOM ambao lengo lake ni kuisaidia serikali kuu na kuzuia juhudi za al-Shabaab kuiangusha.