BARAZA la Mitihani la Taifa (Necta) limemtangaza Paul Cosmas Luziga kama mwanafunzi bora wa mwaka 2020 katika matokeo ya kidato cha nne yaliyotangazwa leo Januari 15, 2021.

 

Luziga ambaye ni mwanafunzi mhitimu kutoka Shule ya Sekondari ya Pandahill iliyopo mkoani Mbeya, amechukua taji hilo kutoka kwa Joan Ritte wa Shule ya St Francis aliyekua mwanafunzi bora mwaka 2019.

 

Hiyo ina maana kuwa kwa miaka miwili mfululizo yaani mwaka juzi na 2020, mkoa wa Mbeya umefanikiwa kutoa mwanafunzi bora kitaifa.

 

Mkuu wa shule hiyo, Mtawa Zephania Lusanika, amesema Luziga alionyesha matokeo mazuri tangu alipojiunga na kidato cha kwanza katika mtihani wa majaribio ya kujiunga na shule hiyo.

 

“Hadi anamaliza shule, Paul alikuwa kati ya wanafunzi watatu bora wa shule. Tulitarajia atafaulu lakini siyo kwa kiwango ambacho amekifikia,” ameeleza mwalimu huyo.

 

Paul amesema ana furaha isiyo na mfano na hakuwahi kutegemea kama ataweza kufikia  nafasi hiyo.

 

“Ninasoma sana lakini ninamtegemea Mungu zaidi. Niliamini nitafannya vizuri lakini siyo kwa kiwango hiki,” ameeleza Paul ambaye changamoto ya ugonjwa wa Corona, haikuweza kuingilia kasi yake ya kujisomea na kupata matokeo mazuri.

 

Paul amefaulu kwa daraja la kwanza pointi saba huku akiwa na alama “A” katika masomo yote yakiwemo fizikia, kemia, baiolojia na hisabati.

 

Naye mama mzazi wa Paul, Lucy Mwogella,  amesema mtoto wake alikuwa akimtegemea Mungu na kwa kipindi chote kuelekea katika mitihani ambapo alifunga bila kula akiombea matokeo yake huku familia ikimsisitiza kusoma kwa bidii.

 

“Alikuwa na siku tatu za kuacha kula kila wiki. Ilipofika kipindi cha mitihani, tulimwambia aendelee na mitihani na sisi tutaendelea kuomba,” amesema mama huyo huku akitokwa na machozi ya furaha wakati akiongea muda mfupi baada ya matokeo kutangazwa na Necta.

 

Ameongeza kwamba licha ya kuwa na uwezo mdogo kiuchumi, ataendelea kufanya kila awezalo kwa msaada wa Mungu kuhakikisha ndoto za mtoto wake zinatimia.

 

“Hali yetu ni ya kawaida kwani hatuna wa kumtegemea maana baba yake alifariki tangu mwaka 2018. Kwa sasa Paul anasomeshwa na kaka yake,” amesema Lucy.