Na Prisca Ulomi,WMTH
Waziri wa Mawasiliano na Teknolojia ya Habari, Dkt. Faustine Ndugulile amefunga kikao cha Mameneja wa Mikoa yote ya Shirika la Mawasiliano Tanzania kilichofanyika Dodoma kwa muda wa siku tatu ambacho kimehudhuriwa na Katibu Mkuu wa Wizara hiyo, Dkt. Zainab Chaula, Naibu Katibu Mkuu, Dkt. Jim Yonazi, Menejimenti ya Wizara na wa TTCL na wawakilishi wa taasisi zilizo chini ya Wizara hiyo

Dkt. Ndugulile ameipongeza TTCL kwa kujiwekea malengo ya kuboresha utendaji kazi wa Shirika hilo na kuazimia kuongeza idadi ya wateja kutoka asilimia 2 hadi asilimia 6 kwa mwaka mmoja wanaotumia simu za mkononi waliopo kwenye soko; kuongeza idadi ya mawakala wa vocha na wa huduma za fedha mtandao za T – PESA kutoka 2,800 hadi 3,080 katika kipindi cha miezi mitatu; na kuboresha mifumo ya utoaji huduma kwa wateja

Amesema kuwa imejitokeza tabia ya baadhi ya taasisi za umma kutumia huduma za TTCL bila kulipa na amemwelekeza Mkurugenzi Mkuu wa TTCL, Waziri Kindamba kuziandikia taasisi zinazodaiwa kuwa walipe madeni yao vinginevyo ifikapo tarehe 31 Januari, 2021 wazikatie huduma hizo  

Ameilekeza TTCL kuchukua hatua kwa watu wanaohujumu miundombinu ya TEHAMA ya TTCL na kudhoofisha ubora wa huduma zake; kuboresha mifumo ya kuhudumia wateja ili kuongeza imani ya wateja kwa Shirika; kuangalia upya mikataba inayoigharimu Shirika ambayo imesainiwa baina ya TTCL na watoa huduma; wajiandae kuingia mikataba baina ya Wizara na Mkurugenzi Mkuu wao na Mameneja ili kupima utendaji kazi; na waongeze ubunifu na kufanya utafiti wa masoko ya huudma za bidhaa zinazotakiwa na wateja

Katibu Mkuu wa Wizara hiyo, Dkt. Zainab Chaula amesema kuwa Wizara na taasisi tukipanga kwa pamoja inakuwa rahisi kuratibu, kusimamia na kufuatilia utekelezaji wa malengo na maazimio tuliyojiwekea ya kuhudumia wananchi na Naibu Katibu Mkuu wa Wizara hiyo ameikumbusha TTCL kuhakikisha kuwa wanajali mazingira ya kazi ya wafanyakazi wa TTCL ili kuwaongezea ari, morali na motisha ya kuwahudumia wateja

Mkurugenzi Mkuu wa TTCL, Waziri Kindamba amesema kuwa wamejipanga kutekeleza maazimio na malengo waliyojiwekea ili kuomgeza huduma na bidhaa za mawasiliano kwa wananchi

Imetolewa na Kitengo cha Mawasiliano Serikalini
Wizara ya Mawasiliano na Teknolojia ya Habari