Mkuu wa Wilaya ya Nyasa Mh. Isabela O. chilumba, amewataka Wajasiliamali na wafanyabiashara wa Wilaya ya Nyasa kufanya biashara halali, na kulipa kodi halali, pia kuacha kuingiza bidhaa kutoka nje ya Nchi na kukwepa kulipa kodi.

Ameyasema hayo hivi karibuni, wakati akiongea na wafanyabiashara wa Wilaya ya Nyasa katika kikao cha kujadili mambo masuala ya Biashara na maendeleo, kikao hicho kilichofanyika Ukumbi wa Baylive uliopo Mbamba bay Wilayani hapa.

Chilumba amefafanua kuwa, wafanyabiashara na wajasiliamali wa Wilaya ya Nyasa wanakabiliwa na changamoto ya ukwepaji ulipaji kodi, na kuingiza bidhaa mbalimbali, kutoka Nje ya nchi hususani,  Msumbiji na Malawi kwa njia za panya ili kukwepa kulipa kodi halali ya Serikali, na kuikosesha nchi yetu Mapato ambayo yangeweza kujenga miundombinu ya Nchi.

Aliongeza kuwa amelazimika kuitisha kikao hicho, ili aweze kutoa elimu kwa wafanyabiashara hao, ili waweze kupata elimu ya ulipaji kodi, na kutoa agizo la kuacha mara moja tabia ya kuingiza kiholela kwa njia za magendo bidhaa mbalimbali kama vile mafuta ya kupikia, yanayotoka Nchini Msumbiji na Sukari inayotoka Nchi ya Malawi.

Aidha amewataka wajasiriamali  kufuata kanuni, taratibu na sheria za kuingiza bidhaa hizo kutoka nje ya Nchi kwa kukata leseni.

“Tunachangamoto kubwa ya Wafanyabiashara wengi ya kuingiza bidhaa mbalimbali kutoka Nchi ya Msumbiji na Malawi, hasa Sukari na Mafuta ya kupikia, ambayo huingia kwa njia isiyokuwa halali na kukwepa kulipa Kodi. Nichukue fursa hii kuwaambia kuwa majina ya wafanyabiashara hayo tunayo na tumekuwa tukikamata na kutaifisha pamoja na wahusika kuwachukulia hatua kali za kisheria, lakini bado wanaendelea kufanya biashara haramu. kama Serikali tuna wajibu wa kutoa elimu kwa Wafanyabiashara, ili wafuate Taratibu kama tulivyoamua kuwaita kwa siku ya leo. Ili Nchi ipate mapato ni Lazima Kila mfanyabiashara walipe kodi halali, na tutahakikisha tunawachulia hatua za kisheria, wale wote watakaokwepa kulipa Kodi ya Serikali.Alisema Chilumba.

Aidha katika hatua nyingine amewapongeza wafanyabiashara hao kwa kuchangamkia fursa za Kibiashara wilayani Nyasa kwa kuleta Bidhaa Mbalimbali na kuhakikisha kila aina ya bidhaa inapatikana katika Wilaya ya Nyasa hususani katika Mji wa Mbamba bay Ambao ni makao makuu ya Wilaya ya Nyasa.

Kwa upande wao wafanyabiashara Wilayani hapa, wameiomba Serikali ya Tanzania, kupunguza ushuru na Tozo hasa katika Bidhaa za Nje kwa kuwa kinachosababisha wakwepe kulipa kodi ni kiwango kikubwa cha tozo wanachotozwa na Mamlaka ya Kodi Tanzania (TRA)  hali inayowapelekea wafanyabiashara hao kutopata faida.

Wameongeza kuwa kama Serikali itaweka viwango rafiki vya ulipaji kodi ya Bidhaa zinazoingia toka Nchi jirani itasaidia kufuata sheria kanuni na Taratibu za ulipaji kodi.

Kwa upande wake Afisa Biashara wa Wilaya ya Nyasa Zaitun Hamza, amewataka wafanyabiashara hao kufahamu kuwa viwango vya  kodi wanazotozwa, ni kwa mujibu wa Sheria ya Kodi hivyo hakuna anayeweza kupunguza viwango hivyo vya kodi. Aidha amewahamasisha wafanyabiashara hao kununua na kuuza bidhaa zinazozalishwa ndani ya nchi ili kukuza uchumi wa Nchi yetu.

Imeandaliwa na Netho c.sichali

Afisa habari wilaya ya Nyasa