DC Chongolo Aridhishwa Na Kasi Ya Ujenzi Wa Vyumba Vya Madarasa Manispaa Ya Kinondoni
Mkuu wa Wilaya ya Kinondoni, Mhe. Daniel Chongolo ameipongeza Manispaa ya Kinondoni kwa kufanikisha kwa asilimia kubwa mpango wa utekelezaji wa miradi ya ujenzi wa vyumba vya madarasa 110 ikiwa ni katika kuhakikisha kwamba wanafunzi walio ongezeka mwaka huu wanapata madarasa ya kusomea.
Pongezi hizo zimetolewa jana wakati wa ziara yake ya kukagua miradi hiyo ambayo inatarajiwa kukamilika mwishoni mwa mwezi huu ambapo pamoja na mambo mengine amesema kuwa Manispaa chini ya Mkurugenzi wake Ndugu. Aron Kagurumjuli wametekeleza adhma hiyo kwa vitendo.
Mhe. Chongolo ameongeza kuwa madarasa hayo yatazinduliwa Februali tano mwaka huu ikiwa ni siku muhimu ya kumbukumbu ya kuzaliwa kwa Chama Cha Mapinduzi CCM na hivyo kuanza kutumika.
Ameongeza kuwa Manispaa ya Kinomdoni inazitendea haki pesa zinazotokana na mapato ya ndani jambo linalopelekea kuwepo na mafanikio makubwa ya miradi inayoanzishwa kwani imekuwa ikikamilika pasipokuwa na changamoto yoyote.
“ Kwa hili nikupongeze Mkurugenzi pamoja na timu yako, kuna watu katika Halmashauri nyingine unafanya ziara ya kukagua mradi fulani lakini ukifika hakuna hata tofali ambalo linaweza kukupa moyo kwamba kunakitu ambacho kinaendelea, ila hapa Kinondoni leo nimeshuhudia kuona madarasa ambayo tulikubaliana yanajengwa na kweli yapo na mengine wanafunzi wanatumia” amesema Mhe. Chongolo.
Awali Kaimu Mkurugenzi Maduhu Kazi alimueleza Mkuu wa Wilaya Chongolo kuwa Manispaa inajenga madarasa 110 yenye thamani ya shilingi zaidi ya Bilioni mbili ambapo kati yake madarasa 46 ni ya shule ya msingi na madarasa 64 ni ya Sekondari ambayo yote yatakamilika mwisho mwa mwezi huu na hivyo kuanza kutumika na wanafunzi.
Mstahiki Meya wa Manispaa hiyo Mhe. Songoro Mnyonge amesema kuwa mafanikio hayo yanatokana na kuwepo kwa uongozi imara wa Mkurugenzi Kagurumjuli kwani amekuwa akitumia fedha za makusanyo ya ndani kwa ajili ya kufanikisha miradi ya maendeleo kwa umaridadi mkubwa.
Ziara hiyo ilihuisha kamati ya ulinzi na usalama ya Wilaya, viongozi wa Chama Cha Mapinduzi ngazi ya Wilaya, mstahiki Meya, Kaimu Mkurugenzi, Wakuu wa Idara pamoja na wataalamu mbalimbali.