Naibu Waziri wa Ujenzi na Uchukuzi, Mhandisi Godfrey Kasekenya, amezitaka Mamlaka mkoani Rukwa kusimamia kikamilifu Sheria ya Mazingira ya mwaka 2004 inayozuia shughuli za kibinadamu katika maeneo ya hifadhi ili kulinda barabara na madaraja katika bonde la mto Rukwa.

Amesema hayo mara baada ya kukagua barabara ya Ntendo – Muze Kilometa 37 na barabara ya Kasansa – Kilyamatundu Kilometa 175 ambazo zimeathiriwa na mafuriko ya mvua kutokana na shughuli za kibinadamu za ukataji miti, kilimo na ufugaji katika safu za milima ya ukanda wa bonde hilo.

“Wakuu wa Wilaya, Wakurugenzi na Wenyeviti wa vijiji na vitongoji hakikisheni tabia ya uharibifu wa mazingira zinazofanywa na wananchi zinakomeshwa maramoja ili kulinda hifadhi za misitu na miundombinu ya barabara na madaraja”, amesisitiza Mhandisi Kasekenya.

Naibu Waziri huyo amesema zaidi ya shilingi Bilioni 4.4 zimetengwa kwa ajili ya kuhakikisha barabara hizo zilizoko katika bonde la mto Rukwa ambalo ni maarufu kwa uzalishaji wa mazao ya chakula zinakarabatiwa ili kupitika wakati wote wa mwaka na kutoathiri uchumi wa wakazi wa mkoa huo.

Naye Kaimu Meneja wa Wakala wa Barabara (TANROADS) mkoa wa Rukwa,  Mhandisi Jotrevas August, amesema zaidi ya madaraja madogo 19 yamebomolewa na mvua hizo zinazoendelea kunyesha katika ukanda huo na hivyo Wakala umejipanga kuhakikisha kuwa ujenzi wake unaendelea ili kutoathiri huduma ya usafiri katika barabara hizo.

Kwa upande wake Mkuu wa Wilaya ya Sumbawanga Dakta. Khalfan Haule, amemhakikishia Naibu Waziri kwamba kwa kushirikiana na watendaji wa kata na vijiji watahakikisha miundombinu ya barabara na madaraja inayojengwa inalindwa ili ikamilike kwa wakati.

Naibu Waziri Kasekenya yuko katika ziara ya kukagua maendeleo ya ujenzi wa miundombinu katika mikoa ya Mbeya, Songwe, Rukwa na Katavi.