Changamoto Za Wakulima Wa Mkonge Kuwa Historia-Majaliwa
WAZIRI MKUU, Kassim Majaliwa amesema Serikali itahakikisha changamoto zote zilizokuwa zinawakabili wakulima wa zao la mkonge nchini ikiwemo ya kuibiwa mapato hazijirudii.
“Awali wakulima walikuwa wanaibiwa sana jambo ambalo kwa sasa halitojirudia tena kwani Serikali imejipanga ipasavyo kuhakikisha mkulima ananufaika, hivyo tulime mkonge unalipa.”
Aliyasema hayo jana jioni (Alhamisi, Januari 21, 2021) alipozungumza na wananchi baada ya kukagua shamba la mkulima mdogo wa mkonge lililoko Magunga Estate wilayani Korogwe.
Waziri Mkuu alisema miaka ya nyuma Tanzania ilikuwa inashika nafasi ya pili duniani katika kilimo cha mkonge ambapo ilikuwa ikizalisha tani 200,000 kwa mwaka ikitanguliwa na Brazil.
Alisema uzalishaji wa zao la mkonge nchini ulishuka kutoka tani 200,000 kwa mwaka na hadi tani 39,000, Serikali imedhamiria kuongeza uzalishaji na kufikia tani 150,000 ifikapo 2025.
Naye, Mkuu wa mkoa wa Tanga, Martine Shigella alisema awali wakulima wa mkonge walikuwa wakilipwa sh. 50,000 kwa tani kutokana na kuibiwa na watu wasio waaminifu ila baada ya Serikali kati bei imeongezeka hadi kufikia milioni nne.
Mkuu huyo wa mkoa alisema hatua hiyo imefikiwa baada ya Serikali kuamua kusimamia mwenendo wa biashara ya kilimo cha mkonge na tayari wakulima wameanza kupata tija
Kwa upande wake, Kaimu Mkurugenzi wa Bodi ya Mkonge, Saady Kambona alisema wamepokea maombi zaidi ya 2,000 ya wananchi wanaohitaji mashamba kulima mkonge.
Alisema Bodi imepeleka maombi Wizara ya Ardhi Nyumba na Maendeleo ya Makazi kurudishiwa mashamba ambayo yametekelezwa ili wayagawe kwa wananchi.
Alisema kwa sasa hamasa ya kilimo cha mkonge ni kubwa baada ya Serikali kuonesha dhamira ya kulifufua zao hilo na wananchi wengi wamejitokeza wameomba mashamba.
Awali, Mwenyekiti wa Magunga Amcos, Shedrack Lugendo alisema uzalishaji wa mkonge umekuwa mzuri baada ya chama chao kusimamia uzalishaji na Desemba mwaka jana walipata daraja la juu ambalo ni 3L kiasi cha tani mbili baada ya kupita miaka 10.
Akizungumzia kuhusu shamba la mkulima mdogo Estohim Urio ambalo Waziri Mkuu alilitembelea alisema mkulima huyo anamiliki hekta 200 alizopewa na Bodi ya Mkonge.
Mwenyekiti huyo alisema mkulima huyo amefanikiwa kupanda hekta 182 ambazo mkonge mkubwa unaovunwa ni hekta 113 na eneo lenye mkonge mdogo ni hekta 69.