Mgombea wa upinzani wa Uganda Bobi Wine amedai kushinda katika uchaguzi wa rais na kukataa matokeo ya awali yaliyotolewa na Tume ya Uchaguzi yanayoonyesha rais Museveni anaongoza katika kinyang'anyiro hicho.
Bildkombo | Yoweri Museveni und Bobi Wine
"Nina imani kubwa kwamba tumemshinda dikteta. Ninatoa wito kwa Waganda wote kukataa hujma hii. Ni wazi kabisa tumeshinda uchaguzi na tumeshinda kwa mbali. Watu wa Uganda watakataa na lazima wakatae unyang'anyi huu wa wazi wa na sauti yao. Ningependa kuwaomba waganda wote kuwa na matumaini kwamba kupitia uchaguzi huu, tumezungumza, na tumezungumza wazi.''
Hiyo ni kauli ya Bobi Wine aliyoitoa hii leo wakati alipozungumza na waandishi wa habari. Awali mwanamuziki huyo aliyegeukia siasa na kuwa maarufu miongoni mwa vijana na chachu yake ya kuleta mabadiliko, aliandika ujumbe kupitia ukurasa wa Twitter kwamba alikuwa na matumaini ya kushinda licha ya kuwepo na "udanganyifu mkubwa na machafuko" katika uchaguzi na kuwashukuru Waganda kwa kujitokeza kwa wingi kushiriki zoezi hilo.
Mwanasiasa huyo mwenye umri wa miaka 38 hakutoa maelezo ya kina kuhusu tuhuma hizo, ambazo zinatofautiana na kauli ya serikali iliyotolewa Alhamis jioni kwamba uchaguzi umekuwa wa amani. Kulingana na kura zilizokwisha hesabiwa, Museveni anaongoza kwa asilimia 63 wakati Bobi Wine hadi sasa amepata asilimia 28.
Afrika Uganda Wahlen
Wapiga kura nchini Uganda walioshiriki uchaguzi wa rais na bunge
Mwenyekiti wa tume ya uchaguzi Simon Byabakama, aliwahakikishia Waganda kwamba matokeo ya uchaguzi yamewasili kwenye kituo cha taifa cha kuhesabia kura licha ya kutokuwepo huduma ya Intaneti.
Museveniambaye ameiongoza Uganda kwa takribani miaka 35, hajatoa kauli yoyote hadi kufikia sasa. Mitaa ya jiji kuu la Kampala ilikuwa kimya hii leo, huku maduka mengi yakiwa yamefungwa. Wanajeshi wameendelea na doria kwenye mitaa mbalimbali.
Marekani, Umoja wa Ulaya, Umoja wa Mataifa na makundi ya haki za binadamu yameelezea wasiwasi juu ya uadilifu na uwazi wa uchaguzi. Uchaguzi wa Uganda ulifanyika wakati serikali ikizima intaneti na mitandao yote ya kijamii. Huduma za intaneti zimeendelea kufungwa leo kwa siku ya tatu mfululizo. Kampeni za uchaguzi nazo ziligubikwa na ukandamizaji wa wapinzani na wafuasi wao uliofanywa na vikosi vya usalama.
Umoja wa afrika ndio taasisi pekee ya kigeni ambayo imewatuma waangalizi, likiwemo kundi la waangalizi wanawake. Siku ya Jumatano Marekani ambayo ni mfadhili mkuu wa Uganda ilitangaza kusitisha ujumbe wake wa waangalizi baada ya wajumbe wake wengi kunyimwa vibali vya kufuatilia uchaguzi. Matokeo kamili ya kura yanatarajiwa kutolewa kesho Jumamosi.