BILIONEA  wa China, Jack Ma inasemekana hajulikani alipo baada ya kutoonekana hadharani kwa zaidi ya miezi miwili.

 

Aidha, alishindwa kuhudhuria onyesho lake la ‘Africa’s Business Heroes,’ Novemba 2020, na aliwakilishwa na mmoja wa wakurugezi wa kampuni la Alibaba Group.

 

Kutoonekana kwake kunakuja wakati serikali ya China inazidi kuzibana biashara zake, baada ya bilionea huyo kuukosoa mfumo wa serikali katika kudhibiti biashara.

 

Kati ya mwaka 2016 na 2017, wakati wa zoezi la kuupiga vita ufisadi nchini China, mabilionea kadhaa walipotea, ambapo wengine walikuja kuonekana wakisema walikuwa ‘wakiisaidia serikali’ ambapo wengine kamwe hawakurejea.

 

Watu maarufu, miongoni mwao ni mfanyabiashara mwenye asili ya China na Canada, Xiao Jianhua, anayemiliki mradi wa Tomorrow Holding, alichukuliwa hotelini kwake jijini Hong Kong na watu waliodaiwa maofisa usalama wa China wakati wa kusherehekea Mwaka Mpya wa China wa 2017.

 

Ripoti zinasema bado anashikiliwa na atafunguliwa mashtaka kwa makosa ya kibiashara na rushwa.