RAIS wa Marekani Joe Biden amezunguza kwa njia ya simu na mwenzake wa Urusi, Vladimir Putin, na kujadili masuala kadhaa ikiwemo mkataba wa kudhibiti silaha na kuwekwa kizuizini kwa Alexei Navalny.

Kulingana na Ikulu ya Marekani, wakati wa mazungumzo hayo  Biden, amemweleza Putin juu ya wasiwasi alionao kuhusu kukamatwa kwa mkosoaji mkubwa wa serikali ya Urusi,  Navalny, tuhuma kuwa Moscow ilihusika na shambulizi la mtandao la hivi karibuni dhidi ya Marekani na madai kwamba Urusi imewalipa wanamgambo kuwaua wanajeshi wa Marekani nchini Afghanistan.

Kwa upande wa Ikulu ya Kremlin yenyewe taarifa yake imejikita kuzungumzia majibu ya Putin kwa pendekezo la Biden la kurefusha mkataba kati ya Marekani na Urusi wa kudhibiti silaha nzito unaofahamika kama New START.

Ijapokuwa taarifa kutoka Washington na Moscow zimetilia uzito mambo tofauti, pande zote  zimeashiria kwamba mahusiano kati ya Urusi na Marekani walau katika siku za mwanzo za utawala wa Biden yataongozwa na shauku ya kutochochea mivutano lakini vilevile bila ya kuharakisha kumaliza tofauti zilizopo baina ya mataifa hayo hasimu tangu enzi ya Vita Baridi.