Kilindi. Mkazi wa Kijiji cha Mvungwe wilayani hapa ameuawa kwa kushambuliwa na ndugu yake baada ya kutokea ugomvi uliotokana na deni la Sh13,000.


Habari zilizopatikana na kuthibitishwa na Kamanda wa Polisi wa Mkoa wa Tanga, Blasius Chatanda ni kuwa mauaji hayo yalitokea jana saa 1:00 asubuhi katika Kitongoji cha Kwesalaka Kijiji cha Mvungwe wilayani Kilindi.


Aliyeuawa katika tukio hilo ni Mahimbo Khatib (40) ambaye anadaiwa kushambuliwa na mdogo wake aliyetajwa kwa jina la Seif Khatib (37)


Watu walioshuhudia tukio hilo walisema ulianza ugomvi baina ya Mahimbo Khatib aliyekuwa akidai Seif Khatib alikuwa anamzungusha kumlipa Sh13,000 alizokuwa akimdai kwa muda mrefu.


“Tulisikia wakizozana baadaye wakaanza kupigana...Mahimbo alianza kukimbia porini lakini Seif akamfuata tulipowafuata kwa ajili ya kuwaamua ugomvi tukakuta Mahimbo analalamika huku akivuja damu kichwani,” alisema Hadija Issah.


Alisema baada ya kuona hivyo, waliamua kumpeleka hospitali na wakati anaendelea na matibabu walipewa taarifa kwamba ameshafariki dunia.


 Kamanda wa Polisi wa Mkoa wa Tanga, Chatanda alisema jeshi hilo linamsaka Seif ili afikishwe kwenye vyombo vya Sheria kujibu shtaka la mauaji.


SIMULIZI ZA MASHUHUDA.


Saidi Muya ambaye ni jirani wa ndugu hao alisema chanzo cha mauaji hayo ni Seif alikwenda nyumbani kwa Mahimbo na alipofika alianza kumdai fedha zake ambazo alimkopesha Oktoba mwaka jana.


“Hawa waliouana ni ndugu mama mmoja na baba mmoja, tunashindwa kujua kwanini walifikia hatua ya kufanya hivi,” alisema Muya.


Shuhuda huyo alisema baada ya ugomvi, Seif alichukua gongo la kuchungia ng’ombe akaanza kumfukuza na alipomkamata alimpiga kichwani mara tatu.


“Alipoona kaka yake kaanguka na hapumui, alitoweka eneo hilo akaenda nyumbani akawabeba watoto wake watatu akawapeleka nyumbani kwa mkwewe akawaacha na kutoroka,” alisema Muya.


Inasemekana kuwa mkewe hakuwepo nyumbani na ndio sababu akachukua uamuzi wa kuwapeleka watoto kwa mkwewe na baadaye kutokomea kusikojulikana.


Athumani Sufian alisema awali majirani walidharau ugomvi huo kwa sababu mara kwa mara, Seif hugombana na kaka yake na mwisho humaliza tofauti zao na kuendelea na shughuli zao.


“Hawa jamaa ni ndugu Seif anafanya shughuli ya kuendesha bodaboda na kaka yake Mahimbo ambaye ni mkulima ilikuwa sio mara yao ya kwanza kugombana. Ilitokea mara nyingi wanazozana halafu wanamaliza tofauti zao na kuendelea na shughuli zao,” aliongeza Athumani.


MAZISHI YALIVYOKUWA


Athumani alieleza kuwa mazishi ya Mahimbo yalifanyika jana saa 9:00 alasiri nyumbani kwao katika Kijijini cha Mavungwe wilayani Kilindi.


Hata hivyo, kinyume na maelezo ya majirani, baadhi ya ndugu wa familia walidai pengine mauaji hayo yalitokana na nguvu za giza.


“Haiwezekani mwanangu amuue hivi hivi kaka yake ni lazima atakuwa alichezewa akili kwa sababu tangu wakiwa wadogo walikuwa wanapendana,” alisema Hussein Daudi, mjomba wa ndugu hao.


Mjomba huyo alidai Mahimbo na Seif wana historia ya kusaidiana kwa hali na mali na kwamba hata Mahimbo alishawahi kumkopesha Seif.