Kampuni ya kutengeneza chanjo AstraZeneca imejiondoa kwenye mkutano na Umoja wa Ulaya kujadili hatua ya kuchelewa kutimiza ahadi yake ya kuupa umoja huo chanjo ya COVID-19. 

Afisa mmoja wa Umoja wa Ulaya amesema hayo.Afisa huyo ambaye hakutaka kutambulishwa jina kwa sababu ya utata unaogubika mazungumzo hayo amesema Umoja wa Ulaya utasisitiza kampuni hiyo kurudi kwenye meza ya mazungumzo kueleza sababu za ucheleweshaji huo punde tu chanjo hiyo inayotengenezwa kwa ushirikiano na chuo kikuu cha Oxford kuidhinishwa na mamlaka inayosimamia dawa Ulaya.

Mazungumzo hayo na Halmashauri Kuu ya Umoja wa Ulaya pamoja na mataifa wanachama wa umoja huo, yamepangwa kwa mara ya tatu mnamo wakati nchi zilizoghadhabishwa za Umoja wa Ulaya zikishinikiza kupewa maelezo.

Mnamo Jumatatu, Umoja wa Ulaya ulitishia kuweka vikwazo vikali kuzuia chanjo za COVID-19 ambazo zimetengenezwa ndani ya umoja huo kuuzwa kwenye mataifa au mashirika ya nje.