Aporwa nyumba mbili Mkoani Shinyanga kisa mkopo wa milioni 5
Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (TAKUKURU) Mkoa wa Shinyanga imefanikiwa kurejesha nyumba mbili zenye thamani ya Sh milioni 55 za Mjasiriamali, Josephine Edward Kiyuga mkazi wa Viwanja vya Mwadui Manispaa ya Shinyanga zilizokuwa zimechukuliwa isivyo halali kampuni ya kutoa mikopo ya Msilikare.
Akitoa taarifa ya Robo ya Pili ya Mwaka wa fedha 2020-2021 (Oktoba – Desemba) leo Januari 20, mjini Shinyanga, Kaimu Mkuu wa Takukuru Mkoa wa Shinyanga, Francis Luena amesema Mjasiriamali huyo ambaye anafuga kuku alikopa kiasi cha Sh milioni 1.5 Septemba 19, mwaka jana kwa mmiliki wa kampuni ya Msilikare inayojishughulisha na kutoa mikopo katika Manispaa ya Shinyanga na kukubaliana kurejesha kiasi cha Sh milioni 2.1 kwa muda wa mwezi mmoja.
Luena amesema, mnamo Septemba 25, mwaka jana mjasiriamali huyo alikopa tena kwa mmiliki huyo Sh milioni 4 na kutakiwa kurejesha Sh milioni 5.6 kwa muda wa mwezi mmoja lakini mmiliki wa kampuni hiyo alimuandikisha Mkopeshwaji mkataba wa mauziano ya nyumba na siyo mkataba wa ukopeshaji wa fedha.
Hivyo, Jumla ya fedha alizokopeshwa ni Sh milioni 5.5 ambazo alitakiwa kurejesha jumla ya Sh milioni 7.7.
Hata hivyo, Mkopaji alifanikiwa kurejesha Sh milioni 8 kama faida ya riba ya kuchelewesha kulipa deni, lakini mkopeshaji alikataa kurejesha hati za nyumba na kudai kuwa muda wa kurejesha deni ulishapita hivyo kama mkopaji anahitaji nyumba hizo inabidi azinunue tena kutoka kwake kwa gharama ya Sh milioni 19 ili zitimie fedha hizo yaani Sh milioni 19 mkopaji alitakiwa kuongeza Sh milioni 11.
“Baada ya Takukuru kupata malalamiko hayo na uchunguzi kufanyika ilibaini kuwa mkopeshaji alikuwa na nia ya kujipatia nyumba hizo kwa njia isiyo sahihi.
“Hivyo basi, Takukuru Mkoa wa Shinyanga iliweza kuziokoa nyumba hizo na zitakabidhiwa leo (Jumatano) kwa mwananchi huyo,” amesema.
Katika hatua nyingine, Takukuru imerejesha na kumkabidhi Mwalimu Mstaafu Sh milioni 2.45 ikiwa ni sehemu ya Sh milioni 45 zinazoendelea kurejeshwa zilizochukuliwa isivyo halali na wakopeshaji watatu tofauti ambao aliwalipa Sh milioni 52, ambapo tayari Mwalimu huyo alikwishakabidhiwa Sh milioni 26.6 katika kipindi cha Julai na Oktoba, mwaka jana.
Vile vile, Taasisi hiyo imezirejesha Jumla ya Sh milioni 7.6 na kuwakabidhi wananchi mbalimbali waliokuwa wakidaiana wakiwemo wafanyabiashara, mafundi ujenzi na vibarua.