HII ni jino kwa jino! Wakati wenyewe wakijinasibu kuwa hawana kinyongo kati yao, upande wa pili, hesabu zinaonesha kuwa Faustina Charles ‘Nandy’ na Zuhura Othuman ‘Zuchu’ wamezidi kuumana kupitia kazi zao, RISASI JUMAMOSI linakujuza.


 


Iko hivi, Zuchu ambaye hana muda mrefu kwenye gemu, alipotoka tu kimuziki, nyimbo zake zilianza kushindanishwa na za Nandy na mjadala ukawa mkali sana kwenye mitandao ya kijamii.


 


Sasa habari mpya ni kwamba, hivi karibu wawili hao wamejikuta kwenye mtanange mkali baada ya kila mmoja kuachia wimbo wake na kufanya vizuri kwenye mtandao maarufu kwa kazi za wasanii, YouTube.


 


Awali, Oktoba 16 Zuchu ndiye alitangulia kwa kuachia audio ya wimbo wake wa Nobody ambao amemshirikisha msanii kutoka Nigeria, Joeboy.


 


Mwezi mmoja baadaye (Novemba 16), Nandy aliingia na miguu yote miwili, akaachia audio na video ya wimbo wake wa Nibakishie akiwa na Mfalme wa Bongo Fleva, Ali Saleh Kiba ‘Alikiba’ ambao nao ukajikusanyia ‘kijiji’ chake huko YouTube.


 


Ndani ya muda mfupi (mpaka juzi Desemba 3), Nandy alikuwa amejikusanyia watazamaji 2,540,244 wakati Zuchu alishafanya balaa zito kwani wimbo wake ulikuwa umeshatazamwa na watu 3,599,738.


 


Licha ya kwamba Zuchu alitangulia kutoa wimbo huo lakini bado inadhihirisha kwamba, Nandy asipouwa makini anaweza kujikuta anasugua benchi kwa mrembo huyo ambaye hana muda mrefu kwenye gemu.


 


Kutokana na ukongwe wake, Nandy alitakiwa afanye balaa la kuwa na watazamaji wengi ndani ya muda mfupi pengine kumzidi Zuchu lakini hata hivyo dalili zinaonesha hana jeuri hiyo na badala yake, Zuchu anaendelea kutamba huko mjini YouTube.


 


Mchambuzi wa masuala ya kiburudani, Aziz Hashim alipozungumza na RISASI JUMAMOSI alisema, nyimbo za Zuchu kwa sasa ni nyingi na kwa ujumla wake zinamuwashia taa nyekundu Nandy.


 


“Zuchu ana nyimbo nyingi kali na zinatamba sana huko YouTube, kuna uwezekano mkubwa sana ukija kupiga mahesabu ya jumla, Zuchu akapata mashabiki wengi zaidi kuliko Nandy,” alisema Aziz.


 


STORI: MWANDISHI WETU