KIKOSI chake kikitarajiwa kujitupa kwenye Uwanja wa Kambarage, Shinyanga leo kuvaana na Mwadui FC, Kocha Mkuu wa Yanga, Mrundi, Cedric Kaze hataki masihara kwa sasa kwani amepanga kutumia wachezaji wake wote nyota ili kuhakikisha anapata ushindi.

 

Mrundi huyo katika michezo ya hivi karibuni ameonekana kutofanya mabadiliko ya kikosi chake cha kwanza kutokana na matokeo mazuri ya mfululizo wanayoendelea kupata.

 

Kikosi hicho ambacho amekuwa akikitumia kinaundwa na kipa Metacha Mnata, Kibwana Shomari, Yasin Mustapha, Lamine Moro, Bakari Mwamnyeto, Mukoko Tonombe, Tuisila Kisinda, Feisal Salum ‘Fei Toto’, Michael Sarpong, Deus Kaseke na Yacouba Songne.


Tarajia kukiona kikosi hicho kikianza katika mchezo huo dhidi ya Mwadui utakaopigwa saa kumi kamili jioni ambacho baadhi ya wachezaji wake wakiwa katika kiwango cha juu akiwemo Yacouba na Tuisila ambao tegemeo katika timu hiyo.

 

Akizungumza na Championi Jumamosi, Kaze alisema kuwa kwake hana mechi nyepesi, hivyo amepanga kuingia uwanjani katika mchezo huo kwa tahadhari kubwa ya wapinzani wake Mwadui.


Kaze alisema kuwa, tayari ameziona video tano za michezo ya ligi iliyopita ya mwisho waliyocheza na lengo kuwajua wachezaji hatari kwa ajili ya kuwadhibiti.“

 

Malengo yangu ni kuona tunamaliza mzunguko wa kwanza tukiwa kileleni tukiwaacha wapinzani wetu kwa idadi kubwa ya pointi, hiyo itatufanya turejee katika mzunguko wa pili kwa morali kubwa ya kuchukua ubingwa katika msimu huu.“

 

Ninaamini tukianza mzunguko wa pili tukiwa kileleni kutapunguza presha kwa wachezaji wangu, hivyo nimefanya maandalizi ya kutosha kuelekea mchezo wetu dhidi ya Mwadui.“

 

Mwadui siyo timu nyepesi, hivyo kikosi changu hakitakuwa na mabadiliko yoyote na zaidi nitaendelea kuwatumia wachezaji waliocheza mchezo uliopita hiyo baada ya kuridhishwa na viwango vya wachezaji wangu walivyokuwa navyo,” alisema Kaze.

Kwa upande wa Kocha wa Mwadui FC, Khalid Adam, alisema kuwa: “Siwezi kuwaza ni mbinu gani nitakazowapa wachezaji wangu kwenye mchezo huo kwani wanapocheza na timu kubwa wenyewe wanatamani kucheza na timu za aina hiyo.“

 

Kila mmoja anapenda apangwe kwani wanapata nafasi ya kujitangaza, lakini pia wanakutana na wachezaji wenye uwezo na kila mmoja anaonyesha uwezo wake.”Mwadui inashika nafasi ya pili kutoka mwishoni mwa msimamo wa ligi baada ya kucheza michezo 14 wakivuna pointi 10.

GPL