KIUNGO mshambuliaji wa Yanga, raia wa Burkina Faso, Yacouba Songne, ameweka rekodi nzuri katika timu hiyo ya kuwa kinara wa kupiga pasi za mabao (asisti).

 

Yacouba, ni kati ya viungo wapya waliojiunga na timu hiyo msimu huu, akisaini mkataba wa miaka miwili, akitokea Asante Kotoko ya nchini Ghana.

 

Nyota huyo alianza vibaya katika msimu huu kwa kushindwa kuonyesha kiwango kikubwa huku mashabiki wa timu hiyo wakiponda uwezo wake kabla ya kubadilika katika mchezo wa Ligi Kuu Bara walipocheza dhidi ya Azam FC.Yacouba akiwa anaichezea timu hiyo, amefanikiwa kupisa asisti nne ambazo hakuna mchezaji yeyote alizozifikisha huku akifunga mabao matatu.

Kiungo huyo katika mchezo uliopita wa ligi walipocheza dhidi ya Mwadui, alifanikiwa kuweka rekodi ya kupiga asisti moja huku akifunga mabao mawili kabla ya kutolewa katika kipindi cha pili na nafasi yake kuchukuliwa na Ditram Nchimbi.

 

Kiungo mshambuliaji raia wa DR Congo Tuisila Kisinda na Farid Mussa ndio wanaofuatia ambao wamepiga asisti tatu kila mmoja.Carlinhos ndiye anayefuatia akipiga asisti mbili sawa na Deus Kaseke, aliyerejea katika ubora wake akiwa amefunga mabao matatu kwenye ligi.

 

Wachezaji wengine wanaofuatia wenye asisti moja ni Ditram Nchimbi, Kibwana Shomari na nahodha Lamine Moro.Yanga hadi hivi sasa imefunga mabao 22 huku ikiruhusu mabao matano pekee, ikiwa haijafungwa bao katika mechi 10.

 

Mshambuliaji Michael Sarpong ndiye anayeongoza kwa mabao akiwa amefunga manne.Moro, Kaseke na Yacouba Songne wamefunga mabao matatu kila mmoja huku Carlinhos, Mukoko Tonombe na Tuisila wao wamefunga mabao mawili kila mmoja, wakati Waziri Junior na Haruna Niyonzima wao wamefunga bao moja.