Na Munir Shemweta, WANMM DODOMA
Mkuu wa Kitengo cha Kodi Wizara ya Ardhi Nyumba na Maendeleo ya Makazi Dennis Masami amesema katika kuhamasisha ulipaji kodi ya ardhi na tozo nyingine zinazohusiana na sekta hiyo nchini Wizara imeanza utaratibu wa kumilikisha ardhi kwenye mitaa mbalimbali nchini kwa lengo la kusogeza huduma karibu na wananchi.
Kwa kuanzia huduma imeanza kutolewa kwenye mtaa wa Maganga kata ya Mkonze katika jiji la Dodoma ambapo timu ya Watendaji wa sekta ya ardhi ilikuwa Ofisi ya Mtendaji Kata kwa lengo la kuhamasisha ulipaji kodi na utoaji huduma za sekta ya ardhi ikiwemo kumilikisha wananchi ardhi.
Mkuu wa Kitengo cha Kodi Wizara ya Ardhi Dennis Masami jana akiwa katika zoezi la kuhamasisha ulipaji kodi ya pango la ardhi na tozo nyingine zinazohusiana na sekta hiyo kwa nchi nzima alitembelea Mtaa wa Maganga ilipo Ofisi ya Mtendaji Kata ya Mkonze Dodoma na kujionea utendaji kazi ambapo alionesha kuridhishwa kasi ya ulipaji kodi na umilikishaji ardhi kwenye mtaa huo.
Akizungumza katika ofisi ya Mtendaji alisema, sasa Wizara ya Ardhi Nyumba na Maendeleo ya Makazi imeona umuhimu wa kushusha huduma za ardhi katika ngazi ya mitaa kwa kushirikisha watendaji wa mitaa ili kusaidia utoaji elimu na ukusanyaji maduhuli ya serikali kwa upande wa kodi ya ardhi.
Aliongeza kwa kusema, watendaji wa Kata nchini ni muhimu katika kuhamasisha wamiliki wa ardhi kulipa kodi ya ardhi kwa kuwa wako karibu na wananchi na wizara imeona ni vizuri ikawatumia kwa ushirikiano na watendaji wa sekta ya ardhi katika halmashauri za wilaya na majiji ili kurahisisha zoezi hilo.
Kwa mujibu wa Masami, Wizara ya Ardhi Nyumba na Maendeleo ya Makazi, mbali na watendaji wake kushiriki kutoa elimu kuhusiana na umuhimu wa kulipa kodi ya ardhi na huduma nyingine zinazohusiana na ardhi pia watahakikisha wamiliki wa ardhi wanaofika wanapatiwa Ankara za malipo na kulipia papo hapo kwa taasisi za kibenki ambazo zitakuwepo katika mitaa husika.
‘’Zoezi la kusogeza huduma za ardhi kwenye mitaa litawapunguzia gharama wananchi na kuwafanya kuiona serikali inawajali, kupeleka watendaji kumi kwa ajili ya kuhudumia watu mita tano katika mtaa inasaidia sana kwani hawatakuwa na ulazima wa kuzifuata huduma mbali’’ alisema Masami.
Mmoja wa wananchi waliofika kupata huduma kwenye mtaa wa Maganga Benadicta Kimario aliipongeza Wizara ya Ardhi kwa uamuzi wake wa kusogeza huduma karibu na wananchi na kuelezea uamuzi huo kuwa utasaidia kuondoa kero waliyokuwa wakiipata kufuata huduma ya kumilikishwa na huduma nyingine katika ofisi za mjini.
‘’Mimi nikiwa mjini nilipata taarifa kuwa Wizara imesogeza huduma kwenye mtaa hivyo nikaona nije kuonana na wahusika maana nina kiwanja nataka kuanza kujenga na hapa nimeonana na wahusika na kuhudumiwa, kwa kweli zoezi hili ni zuri sana’’ alisema Benedicta.