Waziri Mkuu Asitisha Likizo Za Krismas Na Mwaka Mpya
*Ni kwa watendaji wa mikoa, wilaya na halmashauri
WAZIRI MKUU Kassim Majaliwa amewaagiza Makatibu Tawala wa Mikoa yote nchini wahakikishe kuwa watendaji wote wa Mikoa, Wilaya, Halmashauri wasiende likizo ya sikukuu ya Krismas na mwaka mpya kwa mwaka huu, badala yake wakasimamie ukamilishaji wa ujenzi wa vyumba vya madarasa na madawati na wawe wamekamilisha ifikapo Februari 28, 2021.
“Suala hili nitalifuatilia mwenyewe ili kuhakikisha wanafunzi wote waliochaguliwa chaguo la kwanza na la pili wawe wameingia madarasani kufikia Machi Mosi mwaka 2021. Ukamilishaji wa vyumba hivyo pamoja na madawati ufanyike kwa kutumia vyanzo vyenu vya ndani vya fedha.”
Waziri Mkuu ametoa agizo hilo jana (Jumatatu, Desemba 7, 2020) alipozungumza na Wakuu wa Mikoa, Katibu Mkuu Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia, Katibu Mkuu Ofisi ya Rais-TAMISEMI. Kikao hicho ambacho Waziri Mkuu alikiongoza kwa njia ya televisheni akiwa ofisini kwake Mlimwa, jijini Dodoma kilihusu upokeaji wa taarifa ya maandalizi ya kupokea wanafunzi wa kidato cha kwanza, 2021.
Waziri Mkuu ameiagiza Ofisi ya Rais-TAMISEMI ihakikishe kazi hiyo inakamilika kwa wakati na amewataka watendaji hao wahakikishe ukamilishaji wa ujenzi wa vyumba hivyo vya madarasa na utengenezaji wa madawati unafanyika usiku na mchana.
Awali, Naibu Katibu Mkuu Ofisi ya Rais-TAMISEMI, Bw. Gerald Mweri alisema kati ya wanafunzi wanaotarajiwa kujiunga na kidato cha kwanza mwaka 2021, wanafunzi 970 watapangwa kwenye shule maalumu, 1,059 shule za ufundi, 1,280 bweni kawaida, 803,326 watapangwa katika shule za sekondari za kutwa.
Kwa upande wake, Mkuu wa Mkoa wa Katavi, Bw. Juma Homera alisema katika mkoa wake wanafunzi wote waliofaulu watapata nafasi ya kujiunga na kidato cha kwanza 2021 kwa sababu awali walikuwa na upungufu wa vyumba 42 vya madarasa, ambapo wamejenga shule mpya saba zenye vyumba 26 vya madarasa na wamekamilisha maboma 56 na hivyo kuwa na ziada ya vyumba 36 vya madarasa.
Kiongozi huyo alisema kuwa mkoa umeweka mkakati wa kuwapeleka wanafunzi wote waliofeli katika vyuo vya maendeleo ya wananchi ili kuwawezesha kupata stadi za maisha zitakazowawezesha kujitegemea. “Mpango huu tunautekeleza kwa awamu ya pili sasa.”
Naye, Mkuu wa Mkoa wa Lindi, Bw. Godfrey Zambi alisema mkoa wake ulikuwa na upungufu wa vyumba 400 vya madarasa, hadi sasa tayari wamekamilisha ujenzi wa vyumba 380 na kwamba watahakikisha hadi Januari 30, 2021 watakuwa wamekamilisha ujenzi wa vyumba vilivyosalia na wanafunzi wote watachaguliwa katika awamu ya kwanza.