Na Shamimu Nyaki –WHUSM,Dar es Salaam
 Waziri wa Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo Mhe. Innocent Bashungwa amesema kuwa katika uongozi wake atahakikisha heshima ya michezo hapa nchini inarejea.

Mhe. Bashungwa ameyasema hayo Desemba 28,2020 Jijini Dar  es  Salaam ambapo alifanya kikao na makocha pamoja na wanamichezo wa zamani na ameeleza kuwa  Serikali imeanza kutenga fedha kwa ajili ya Mfuko wa Maendeleo ya Michezo.

“Lengo la kikao hiki ni kupokea mawazo kutoka kwenu namna bora ya kuendesha michezo ili tupate mafanikio kama ambayo tulipata hapo zamani wakati nyie mkilitumikia taifa letu katika soka” alisema, Mhe. Waziri Bashungwa.

Mhe. Bashungwa ameongeza kuwa marekebisho yaliyofanywa katika Sheria za Baraza la Michezo la Taifa (BMT) ya mwaka 1967 kuhusu michezo ya ridhaa na kulipwa, Kwa hivi  sasa inatambua  michezo ya kulipwa  ambapo kuna wachezaji zaidi ya 2000 wanaocheza michezo ya kulipwa ndani ya nchi na wanamichezo takriban 28 wanacheza michezo ya kulipwa nje ya nchi.

Aidha, Mhe. Waziri Bashungwa amewapongeza wachezaji wa zamani kwa jinsi walivyojituma kwa nidhamu na moyo wa kizalendo kuipigania nchi na kufanikiwa kufuzu  katika mashindano ya AFCON mwaka 1979.

Kwa upande wake Naibu Waziri wa Wizara hiyo Mhe. Abdallah Ulega ameiagiza Idara ya Michezo kusimamia maazimio yote ya kikao hicho kufanyiwa kazi na matokeo yaonekane.

“Nia yetu ni kuendeleza michezo, na hili tutalisimamia vyema hivyo tunaomba mawazo mazuri kutoka kwenu namna ya kuendeleza michezo” alisema Mhe.Ulega.

Mhe. Ulega ameongeza kuwa dhamira ya vikao na wadau wa michezo ni kutathmini michezo ilipotoka, ilipo na wapi ielekee kwa maslahi ya taifa.

Naye Mdau wa michezo michezo Bw. Ally Mayai Tembele ameishukuru Serikali kwa kuandaa vikao vya kukutana na wadau kupokea mawazo kuhusu maendeleo ya michezo nchini, huku akieleza kuwa michezo inahitaji nidhamu na kuwekeza kwa Watoto wa shule za msingi na sekondari, vifaa vya michezo na miundombinu bora ya michezo.