Waziri Bashungwa aiagiza COSOTA kuongeza kasi ya Utendaji
Na Shamimu Nyaki – WHUSM, Dar es Salaam
Waziri wa Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo Mhe. Innocent Bashungwa ameiagiza Taasisi ya Hakimiliki Tanzania (COSOTA) kuongeza kasi katika kutekeleza usimamizi wa kazi za Sanaa.
Mhe. Waziri Bashungwa ameyasema hayo Desemba 23, 2020 Jijini Dar es Salaam alipotembelea Taasisi hiyo akiambatana na Naibu Waziri Mhe. Abdallah Ulega pamoja na Katibu Mkuu Dkt. Hassan Abbasi.
Katika ziara hiyo Mhe. Bashungwa ametoa wiki moja kuanzia leo kwa Taasisi hiyo kuhakikisha wanakuwa na Mpango Mkakati wa namna ya kushughulika na waharamia wa kazi za Sanaa.
“Nawaagiza COSOTA kujitangaza kutumia vyombo vya habari na njia nyingine ikiwemo Mitandao ya kijamii ili mnayotekeleza wadau wenu wayajue” alisema, Waziri Bashungwa.
kwa upande wake Naibu Waziri Mhe. Abdallah Ulega ameiagiza Taasisi hiyo kuongeza juhudi katika kukusanya mapato ya Serikali kupitia sekta ya Sanaa.
Naye Katibu Mkuu wa Wizara hiyo Dkt.Hassan Abbasi ameeleza kuwa, tangu COSOTA ihamie Wizara ya hiyo mabadiliko mbalimbali yaliyohotajika kufanyika yametekelezwa, huku akiongeza kuwa lengo ni kuhakikisha Wadau wa Sanaa wananufaika na kazi zao.
Vile vile Mtendaji Mkuu wa COSOTA Bi. Doreen Sinare amesema kuwa Taasisi hiyo imefanikiwa kuhuisha muundo pamoja na kutatua changamoto mbalimbali zilizokuwa zinawakabili wasanii.