Wawekezaji kutoka nchini Uturuki wamewasili nchini Tanzania kwa ajili ya kujionea fursa za uwekezaji na biashara zilizopo nchini ili waweze kuwekeza na kukuza Diplomasia ya Uchumi baina ya mataifa hayo.

Balozi wa Tanzania nchini Uturuki, Mhe. Prof. Elizabeth Kiondo amethibisha kuwasili kwa wawekezaji hao wakati wa uzinduzi wa Taasisi ya Waturiki "Compass Partners" leo jijini Dar es Salaam, na kuongeza kuwa wawekezaji watano kati ya kumi wamefika nchini na kujumika na waturuki wengine wanaofanya biashara zao hapa nchini.

"Wawekezaji hawa kutoka Uturuki wamekuja na wamefungua taasisi yao inayojulikana kwa jina la "Compass Partners" ili kuendeleza biashara na tunaamini kwa kutekeleza biashara hii tunaenda kuendeleza uchumi wa Tanzania na kutengeneza ajira kwa watanzania," Amesema Prof. Kiondo

Prof. Kiondo ameongeza kuwa, hatua ya kwanza wawekezaji hao wameleta bidhaa mbalimbali ili watanzania wazione, hatua ya pili itakuwa ni uwekezaji wa kiwanda hapa nchini kwa ajili ya kuanza uzalishaji wa bidhaa ambazo zitauzwa hapa nchini.

Aidha, kwa upande wa bidha zinazozalishwa hapa nchini ambazo zina fursa ya kuuzwa Uturuki ni pamoja na chai, pamba, tumbaku na kahawa bidhaa hizi zote zina soko kubwa sana nchini Uturuki.

Tunazalisha tani 350,000 za pamba lakini tunaweza kuchakata asilimia 15 tu, hivyo tumepata tayari mwekezaji ambaye atawekeza katika kiwanda cha nguo mkonani simiyu ili kuongeza thamani ya bidhaa ya pamba hapa nchini.

Balozi, Prof. Kiondo ametoa wito kwa Watanzania kuanza kuchangamkia fursa hizo za biashara ili waweze kuongeza kipato na kuongeza biashara zao.

Kwa upande wake, Kaimu Balozi wa Uturiki hapa Nchini, Mhe. Onur Yah amesema kuwa biashara kati ya Tanzania na Uturiki imekuwa ikiimarika kila wakati kwani Tanzania ni sehemu salama ya kuwekeza na kufanya biashara.

"Kupitia uwekezaji katika sekta mbalimbali ni imani yangu kuwa tutaendelea kukuza na kuimarisha uhusiano wetu wa kidiplomasia," Amesema Mhe. Yah

Aidha, amewataka Waturuki na Watanzania kutumia fursa za biashara zinazopatikana baina ya mataifa hayo ili kufanya biashara na kukuza uchumi wao.

Ushirikiano wa Tanzania na Uturuki ni wa muda mrefu, pamoja na mambo mengine uhusiano huo umekuwa ukijikita zaidi katika kuendeleza uwekezaji wa viwanda, elimu na utalii hasa katika kutangaza vivutio vya utalii vya Tanzania nchini Uturuki.