Washikiliwa kwa kumshambulia kwa ngumi, mateke dereva wa lori
Jeshi la Polisi mkoani Shinyanga linawashikilia watu wanne akiwemo dereva wa basi la Kampuni ya Frester wakituhumiwa kwa kosa la kumshambulia dereva wa lori wakimtuhumu kwa kosa la kutaka kuwasababishia ajali.
Kamanda wa Polisi wa Mkoa wa Shinyanga, Debora Magiligimba amewataja wanaoshikiliwa kuwa ni dereva wa basi la Kampuni ya Frester lenye namba za usajili T.915 CGU, Mwita Chacha mkazi wa wilaya ya Kahama mkoani Shinyanga na abiria wake Joyce Charles.
Abiria wengine waliokamatwa ni Athumani Mussa na Christopher Rangati wote wakituhumiwa kwa kosa la kumshambulia kwa ngumi na mateke dereva wa lori, Emmanuel Msuya mkazi wa Moshi mkoani Kilimanjaro.
Kamanda Magiligimba amesema, tukio hilo lilitokea juzi katika eneo la Samuye wilayani Shinyanga na kwamba chanzo cha vurugu ni dereva wa basi la kampuni ya Frester kulibana ubavuni lori lililokuwa likisubiri kupimwa katika mzani wa kupimia magari uliopo Tinde wilayani Shinyanga.
Akifafanua amesema, lengo la dereva wa basi kulibana lori ni kutaka kupima haraka kabla ya lori ambapo hata hivyo dereva wa lori hakuruhusu basi hilo lipimwe kabla yake na yeye alipima na kuondoka kuendelea na safari bila ya kusababisha ajali yoyote eneo la mzani.