Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa, (TAMISEMI) Mheshimiwa Selemani Jafo amewaagiza Wakurugenzi wa Halmashauri Nne kuandika barua kwa Katibu Mkuu TAMISEMI mhandisi Joseph Nyamhanga kujieleza ni kwanini walishindwa kuwaruhusu wakuu w shule kuhudhuria mkutano wao wa mwaka.

Waziri Jafo, ametoa maagizo hayo Jijini Dodoma wakati alipokuwa akifungua mkutano mkuu wa mwaka wa Chama cha wa wakuu wa shule za sekondari Tanzania bara (TAHOSSA) unaofanyika jijini Dodoma.


Wakurugenzi, ambao hawakutoa ruhusa kwa wakuu wa shule za sekondari kwamujibu wa Jafo ni mkurugenzi wa Halmashauri ya Msalala, Kahama DC, Kologwe DC pamoja na Sikonge.

Amebainisha, kuwa mkutano kama huo ndiyo sehemu ambayo serikali inatumia kutoa maagizo kwa wakuu wa shule katika usimamizi wa masuala mbalimbali ya kielimu katika maeneo yao.

Amesema, serikali ya awamu ya tano imetoa fedha nyingi katika kuboresha miundombinu ya elimu ambayo wasimamizi wakuu ni wakuu wa shule za sekondari hivyo ushiriki wao katika mkutano huo ni jambo la lazima.

“Kuna kiasi kikubwa cha fedha serikali imewekeza katika kuboresha miundombinu ya shule nchini na wasimamizi ni nyinyi wakuu wa shule hivyo uwepo wenu hapa na sisi serikali tunapata fursa yakutoa maagizo yetu lakini sasa kuna baadhi ya wakurugenzi wameshindwa kutoa vibali kwa wakuu wa shule” amesema Jafo.

Kutoka na hali hiyo Waziri Jafo, amemwagiza Katibu Mkuu TAMISEMI, Mhandisi Joseph Nyamhanga kuwachukulia hatua wakurugenzi hao haraka.