Na. Edward Kondela
Wafugaji wametakiwa kuanza kufikiria kuwa na ng’ombe bora badala ya kuwa na ng’ombe wengi wasio na ubora ambao hawakidhi tija katika maisha yao kwa kutotoa mazao bora ambayo hayawezi kutoa kipato cha kuridhisha.

Akizungumza jana (29.12.2020) katika Kijiji cha Kinango kilichopo Wilaya ya Magu Mkoani Mwanza wakati akishuhudia zoezi la uogeshaji mifugo dhidi ya magonjwa mbalimbali wakati wa ziara yake ya siku mbili mkoani humo, Waziri wa Mifugo na Uvuvi Mhe. Mashimba Ndaki amesema mifugo mingi wakiwemo ng’ombe ni njia mojawapo ya kutunza fedha ambayo imekuwa ikitumiwa na wafugaji hivyo ni muhimu wafugaji hao kuhakikisha mifugo yao inakuwa bora kwa kuipatia huduma muhimu ikiwemo ya kuiogesha.

“Nchi yetu tuna ng’ombe wengi sana, lakini wengi siyo bora kama inavyotakiwa sasa tunatakiwa kutoka kuwa na ng’ombe wengi tu bali tuwe na ng’ombe walio bora, tukiwa na ng’ombe wengi wasio bora hawatusaidii sana katika maisha yetu, kwa sababu lengo la kuwa na ng’ombe atupe nyama, atupe maziwa na atupe kipato sasa tufikirie kuwa na ng’ombe bora na moja ya njia ya kuwa na ng’ombe bora ni hii ya kuwaogesha.” Amesema Mhe. Ndaki

Mhe. Ndaki ameongeza kuwa Wizara ya Mifugo na Uvuvi kwa Mwaka wa fedha 2020/2021 imetenga bajeti ya kukarabati majosho kadhaa yaliyopo maeneo mbalimbali nchini na kuahidi kuwa wizara itakarabati majosho matano yaliyopo katika Wilaya ya Magu ili mifugo mingi iweze kuogeshwa na kuwa bora.

Pia, Mhe. Ndaki akiwa ameambatana na Naibu Waziri wa Mifugo na Uvuvi Mhe. Pauline Gekul katika ziara hiyo amesema njia nyingine ya kuwa na ng’ombe bora ni wafugaji kuhakikisha mifugo yao inapata malisho bora ambayo yatafanya mifugo hiyo kuwa na afya bora lakini kwa sasa wafugaji wamekuwa wakichunga katika maeneo machache hali inayofanya mifugo kutokula chakula kinachotakiwa.

Ameongeza kuwa Wizara ya Mifugo na Uvuvi imekuwa ikishughulikia sana suala la malisho ambalo ni moja ya tatizo kubwa kwa wafugaji pamoja na maji na kutumia fursa hiyo kumshukuru Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt. John Magufuli kutokana na kuruhusu wafugaji wachunge kwenye baadhi ya maeneo yaliyokuwa ya hifadhi na mengine kuzuiliwa hali iliyotoa ahueni kwa wizara kupata maeneo ya kulisha mifugo ili iwe na ubora.

Kwa upande wake Kaimu Msajili wa Bodi ya Nyama Nchini (TMB) Bw. Iman Sichalwe amewaeleza wafugaji kuwa suala la kuogesha mifugo dhidi ya magonjwa ni muhimu kwa kuwa limekuwa likizuia Tanzania kuuza nyama katika nchi mbalimbali kutokana na viwanda vya kuchinja na kuchakata nyama kutopata mifugo bora.

Amefafanua kuwa uogeshaji unaboresha afya ya mfugo ikiwemo ya nyama na ngozi hivyo kuvifanya viwanda kufanya kazi na kuwaongezea vipato wananchi kwa kupata masoko ya kuuza mifugo yao, serikali kupata fedha kupitia tozo mbalimbali, upatikanaji wa fedha za kigeni na kwamba hali hiyo haitawezekana endapo mifugo haitadhibitiwa na magonjwa ili kupata nyama bora na kutengeneza bidhaa zitokanazo na ngozi bora.

Katika ziara hiyo ya siku mbili Mkoani Mwanza, Waziri wa Mifugo na Uvuvi Mhe. Mashimba Ndaki ametembelea pia kiwanda cha kuchinja na kuchakata nyama cha Alpha Choice kilichopo wilayani Magu na kuzungumza na baadhi ya wafugaji waliofika kiwandani hapo kwa kuwataka waanze kubadilisha ubora wa mifugo yao kwa kuwachanja, kuwaogesha, kuwapatia maji na malisho yanayotosheleza na kuacha kuwachunga katika maeneo marefu ili mifugo hiyo iwe na afya nzuri ambayo mfugaji atauza kwa bei nzuri na mwenye kiwanda kupata mfugo wenye mazao bora.

Mhe. Ndaki amesisitiza hilo baada ya kupata malalamiko kutoka kwa baadhi ya wawekezaji kwenye viwanda vya kuchinja na kuchakata nyama kutopata ng’ombe bora ambao wanaweza kukidhi katika soko la kimataifa hali ambayo wakati mwingine nyama kukataliwa na baadhi ya nchi kutokana na mifugo kuwa na magonjwa na nyama kutokuwa na ubora unaotakiwa.   

“Nawaombeni sana tuanze kuboresha ng’ombe wetu ili tupate faida ya kuwa na kiwanda hapa na kingine nimekiona kule wilayani Misungwi na chenyewe wanapata ng’ombe kidogo sababu ni hiyo hiyo ng’ombe wetu hawajawa bora sana, sasa wawekezaji hawa wamelazimika wawe wananununa ng’ombe wanawafuga mahali kwanza wanawalisha ili wabadilike sura na afya waliyotoka nayo kwa wafugaji ambao  ni sisi.” Amefafanua Mhe. Ndaki

Waziri wa Mifugo na Uvuvi Mhe. Mashimba Ndaki akiambatana na Naibu Waziri wa wizara hiyo Mhe. Pauline Gekul na Katibu Mkuu anayeshughulikia Uvuvi Dkt. Rashid Tamatamah pamoja na wataalam wengine kutoka wizarani, amemaliza ziara ya kikazi ya siku mbili Mkoani Mwanza ambapo amejionea mambo mbalimbali yanayohusu sekta za mifugo na uvuvi.