DAR: Upepo haujatulia! Wakati Watanzania wakiendelea kufurahia muziki mzuri kutoka kwao, nyuma ya pazia kunafukuta bifu zito kati staa wa Bongo Fleva, Rajabu Abdul ‘Harmonize’ na wafuasi wa lebo yake ya zamani, Wasafi Classic Baby (WCB), Gazeti la IJUMAA linakupakulia habari kamili.

 

Historia inaonesha, Harmonize au Harmo tangu ajiengue Wasafi, amekuwa kwenye msigano wa matukio mbalimbali ambayo kimsingi yanaonesha dhahiri kuwa, hayupo sawa na ama wafuasi wa lebo yake hiyo ya zamani au timu nzima ya Wasafi.

 

MONDI ANASEMA WAKO SAFI…

Kuhusu timu ya Wasafi, bosi wao, Nasibu Abdul ‘Diamond Platnumz’ amekuwa akikaririwa mara kwa mara akisema hana kinyongo na kijana wake huyo ambaye amemtambulisha kwenye gemu na anamtakia kila la heri kwenye mafanikio yake.

 

TUANGALIE TUKIO BICHI

Tukio ambalo ni la hivi karibuni linalotafsiri kwamba hali si hali, linadaiwa kutokea ndani ya Maduka ya Mlimani City jijini Dar ambapo watu wanaodaiwa kuwa ni wafuasi wa Wasafi (Team Wasafi), wanadaiwa kumvaa Harmo na kuanza kumzomea.