Samirah Yusuph
Bariadi.
Kamanda wa jeshi la polisi mkoa wa Simiyu Richard Abwao,amewataka wananchi kuendelea kutoa ushirikiano kwa jeshi la polisi ili kufichua na  kukomesha vitendo vya uhalifu ndani ya mkoa.

Ameyasema hayo alipokuwa akiwasilisha maada ya hali ya usalama ndani ya mkoa katika kikao cha kujadiri dira ya mkoa kwa mwaka 2021 kilichofanyika bariadi mjini desemba 12,2020.

Abwao alisema kuwa ni wakati wa wananchi kujifunza kutoka katika mifano ambayo imefanikisha kufichua uharifu kwani mtoa taarifa ni mtu mhimu na ni wajibu wa jeshi la polisi kuhakikisha anakuwa salama.

"Hali ya usalama katika ni nzuri kwa sababu jeshi la polisi muda wote lipo kazini, niwahakikishie usalama watoa taarifa wetu na kuwaambia kuwa ushirikiano wa polisi na wananchi ni muhim sana katika kuhakikisha usalama wa raia" alisema Abwao na kuongeza kuwa:

"Kwa sasa jeshi la polisi lizidi kuimarisha ulinzi kwa kupeleka askari kwenye kila kata ili washirikiane na watendaji wa vijiji na kata katika kurahisisha upatikanaji wa taarifa na kuwa karibu na wananchi".

Kwa upande wake Ofisa wa jeshi la uhamiaji mkoa wa Simiyu Mariam Mwanzalima amewaonya wananchi wa mkoa huo kujihusisha na vitendo vya udanganyifu wa upatikanaji wa uraia.

Alisema kuwa kumekuwepo na tabia kwa baadhi ya wananchi kushiriki uhalifu huo kwa kuwadaganganya wageni wanaoingia nchini kinyume cha sheria na kuwaharalisha kuwa raia.

Mwisho.