Na Richard Mwaikenda, CCM Blog, Dodoma
WANANCHI wamegombea kununua nyama pori wakati wa uzinduzi wa bucha ya kwanza ya kuuza nyama pori eneo la Chang'ombe, jijini Dodoma Desemba 20,2020.

Tukio hilo lilitokea asubuhi kabla hata ya Mamlaka ya Usimamizi wa Wanyama Pori Tanzania (TAWA), kuzindua rasmi, ambapo wananchi walifurika kwenye bucha hiyo inalomilikiwa na mtu binafsi kila mmoja akitaka kununua nyama hiyo iliyokuwa inauzwa kilo moja sh. 5000.

Ilibidi wahudumu wapate wakati mgumu, hivyo kuamua  kuwaorodhesha kwa majina na kila mmoja kiasi anachotaka lakini isizidi kilo mbili ili kila mmoja apate.

Uzinduzi huo ulifanywa na Mwenyekiti wa Bodi ya Wakurugenzi wa TAWA, Meja Jenerali mstaafu, Hamisi Semfuko ambaye naye alinunua kilo mbili na kupatiwa risiti ikiwa ni ishara ya uzinduzi wa duka hilo. Wajumbe wengine wa Bodi walinunua nyama hiyo wakiwemo wanahabari.

Akizungumza wakati wa uzinduzi huo, Semfuko alisema kuwa TAWA imeamua kuzindua duka hilo kuitikia maelekezo ya Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dk. John Magufuli ya kufungua bucha za aina hiyo kwa nchi nzima, ili wananchi wawe wanafaidi rasilimali za nchi yao.

Alisema  bucha hiyo ni ya kwanza na wataendelea kufungua zingine katika mikoa yote ya Tanzania, pia Tawa ambayo ni msimamizi mkuu wa uwindaji wa wanyama pori nchini, itatoa leseni chache kwa watakaohitaji kuwa na mashamba ya ufugaji wa wanyama pori.

Pia, alisema kuwa TAWA itagawa mitamba kwa watakaokuwa wanaanzisha mashamba hayo, ili uzalishaji uwe mkubwa nyama ipatikane kwa wingi.

Alipoulizwa ni wanyama gani watakaokuwa wanawindwa kwa ajili ya nyama, Semfuko alijibu kuwa ni wanyama wote wanaolika  nyama yao itauzwa kwenye mabucha hayo.

Alitaja nchi zingine za Afrika zizoruhusu wananchi wake kuwa na mashamba ya kufuga wanyama pori kuwa ni; Afrika Kusini, Zimbabwe na Namibia, hivyo kuwataka watanzania kuchangamkia fursa hiyo.

Baadhi ya wananchi waliohojiwa na mwandishi wa habari hizi,hawakuficha furaha yao ambapo waliishukuru serikali  na hasa Rais John Magufuli kwa kuwakumbuka kupata kitoweo hicho adimu.

Mariam Damas (34), mkazi wa Chang'ombe ambaye alikutwa akisubiri zamu yake kununua nyama, alisema kuwa  tangu azaliwe hajawahi kula nyama pori, hivyo  kuishukuru serikali kufungua bucha ya aina hiyo na kwamba yeye na familia yake siku hiyo wataifaidi nyama hiyo.

"Tunashukuru ana serikali kutufungulia bucha hii ya wanayama pori, mi nilikuwa naikia tu kuwa kuna nyama pori, tangu nizaliwe ijawahi kula, nasikia ni tamu sana, ila leo mimi na familia yangu tutakula kwa mara ya kwanza," alisema Mariam.

Mzee Joseph Barabara mkazi wa Mjimwema, Dodoma anayekisiwa kuwa na umri wa zaidi ya miaka 70, alikutwa akishangaa umati uliofurika na kuuliza kulikoni? alipoambiwa ni hafla ya uzinduzi wa bucha ya kuuza nyama pori, alishukuru na kunyoosha mikono yake juu, alipoambiwa bei ya kilo moja ni h. 5000, alisema uwezo wake ni mdogo anachoweza kununua ni utumbo ambao bei yake anaweza kuimudu.