Na. Erick Mwanakulya
Wakala wa Barabara za Vijijini na Mijini (TARURA), unaendelea kutekeleza miradi mbalimbali katika Mkoa wa Njombe ili kuwezesha wananchi kusafiri na kusafirisha bidhaa na mazao kwa urahisi kwa kipindi chote cha mwaka.

Akielezea utekelezaji wa miradi mbalimbali, Mratibu wa TARURA Mkoa wa Njombe, Mhandisi Ibrahim Kibassa ameeleza kuwa ujenzi wa Barabara kwa kiwango cha Lami zinazotokana na Ahadi za Mhe. Rais umekamilika kwa asilimia 100 katika Halmashauri ya Wilaya ya Ludewa, Halmashauri ya Mji wa Makambako na kwa upande wa Halmashauri ya Mji wa Makete barabara hizo zimekamilika kwa asilimia 80.

“TARURA Mkoa wa Njombe inaendelea na utekelezaji wa miradi mbalimbali katika Wilaya zote 4 pamoja na Halmashauri zote, kwa sasa tupo katika ujenzi wa Daraja la Luhuji lenye urefu wa Mita 22 lililopo Njombe Mji ili kuunganisha   Kata ya Ramadhan pamoja na Kata ya Mabatini, daraja hili limegharimu Shilingi Milioni 514”, alisema Mhandisi Kibassa.

Aidha, ameeleza kuwa daraja hilo la Luhuji lilitakiwa kukamilika mwezi Novemba, 2020 lakini kutokana na changamoto za mvua Mkandarasi ambaye ni Pripam Company Ltd ameongezerwa Kipindi cha Mwezi mmoja ili aweze kukamilisha ujenzi wa daraja hilo.

Naye, Mwenyekiti wa Mtaa wa Ramadhan Bw. Festo Mwimba amesema kuwa, mtaa huo umekuwa na changamoto ya ukosefu wa daraja kwa muda mrefu na wamekuwa wakipata wakati mgumu kipindi cha masika hasa wanafunzi wa shule kuvuka kwenda upande wa pili hali iliyopelekea wengine kupoteza maisha na ameipongeza TARURA kwa kujenga daraja hilo la kudumu ili kutatua kero za wananchi.

Wakizungumza katika mahojiano maalum kwa nyakati tofauti Meneja wa TARURA katika Halmashauri ya Wilaya ya Makete, Mhandisi John Kawogo alisema kuwa kabla ya TARURA kuanzishwa maeneo mengi yalikuwa hayawezi kupitika na wananchi wa Matamba, Kinyiko pamoja na Kikondo walishindwa kusafirisha mazao yao, ambapo kwa sasa barabara zote zinapitika kipindi chote na eneo linaloonekana kuwa korofi TARURA inafika kwa wakati ili kufanya matengenezo na kuhakikisha wananchi wanapita bila usumbufu.

“Kuna maeneo yalikuwa hayapitiki kabisa kama Kijiji cha Kipengele, eneo lile ulikuwa huwezi kupita ila kwa sasa barabara zinapitika kwa kipindi chote cha mwaka mzima”, alisema Mhandisi Kawogo.

Naye, Imaculata Msigwa Mkazi wa Mji wa Makambako, ameipongeza TARURA kwa kujenga barabara kwa kiwango cha lami na kwamba kwa sasa ni rahisi sana wananchi kufikisha mazao yao sokoni hasa katika Soko la Nyanya.

Wakala wa Barabara za Vijijini na Mijini (TARURA) katika Mkoa wa Njombe unaendelea kusimamia Mtandao wa Barabara zenye urefu wa Km 5208.58 katika Halmashauri zote 6 ili ziweze kupitika  kipindi chote cha mwaka kwa kutekeleza ujenzi wa mifereji, vivuko pamoja na maboresho ya miundombinu hiyo.