Na Mwandishi wetu, Manyara
MWENYEKITI wa Mtaa wa Miyomboni Mjini Babati, Mathias Zebedayo amefikishwa kwenye Mahakama ya Hakimu Mkazi Mkoa wa Manyara na Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa, TAKUKURU na kusomewa mashtaka ya kuomba na kupokea rushwa ya shilingi laki moja.
Akisoma hati ya mashtaka mjini Babati Desemba 23 mbele ya Hakimu mfawidhi wa mahakama hiyo Simon Kobelo, mwendesha mashtaka wa TAKUKURU Evelyne Onditi amesema Zebedayo anadaiwa kupokea rushwa ya shilingi laki moja kinyume na kifungu cha 15 cha sheria ya kuzuia na Kupambana na Rushwa 11/2007.
Onditi amesema katika kesi hiyo namba 210/2020 Zebedayo alichukua bila halali kiwanja kilichopo mtaa wa Miyomboni na alipoulizwa na msimamizi wa kiwanja akadai kuwa kimetwaliwa na Halmashauri ya mji hivyo atoe shilingi laki moja ili amsaidie kurejesha.
Amesema baada ya TAKUKURU kupokea malalamiko hayo iliweka mtego na Mwenyekiti huyo akakamatwa kwa kupokea kiasi hicho cha shilingi laki moja kilichotegeshwa.
Mwendesha mashtaka huyo wa TAKUKURU ameiambia mahakama hiyo kuwa uchunguzi wa shauri hilo umeshakamilika.
Mshatikiwa huyo Zebedayo hata hivyo, amekanusha mahakamani hapo alipoulizwa kama ni kweli ametenda kosa hilo na Hakimu Kobelo ameahirisha kesi hiyo hadi Januari 26 mwaka 2021.
Mkuu wa TAKUKURU Mkoani Manyara, Holle Joseph Makungu amesema uchunguzi wa kiintelijensia umeonyesha kuwa Zebedayo alikuwa anatumia vibaya jina la mbunge wa jimbo la Babati Mjini kwa kuwatisha wananchi na kujipatia viwanja.
Makungu amesema wananchi wanne waliamini kutokana na matisho hayo hivyo wakakaa kimya hadi Zebedayo alipokamatwa na wao ndipo wakajitokeza kulalamika na malalamiko yao yanachunguzwa.
Amesema wanataka wana Manyara wafahamu kuwa TAKUKURU imepewa majukumu ya kuchunguza na kuchukua hatua na kuhakikisha wanapata haki kwa mujibu wa sheria bila kujali mahali wanapotokea, makabila yao, maoni yao ya kisiasa, rangi zao, jinsia, dini zao au hali zao za kimaisha kama ilivyoainishwa katika kifungu cha 7 cha sheria ya kuzuia na kupambana na rushwa namba 11, 2007 kikisomeka pamoja na ibara ya 13 (5) ya Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ya mwaka 1977 ambayo ndiyo mkataba wa wananchi na Serikali yao.
Ametoa rai kwa wana Manyara kutambua kuwa wala rushwa bado wapo miongoni mwa watumishi wa umma, wanaojipatia manufaa kwa kupitia majina ya viongozi au kujifanya watumishi wa TAKUKURU au vyombo vingine vya usalama na pia bado wapo.
Amewataka wananchi waendelee kutoa taarifa Kwenye ofisi za TAKUKURU au kupiga namba 113 ambayo hailipiwi ili hatua kali zichukuliwe dhidi yao kama ilivyofanyika kwa Zebedayo.