MFANYA-BIASH-ARA anaye-tajwa kuwa ndiye tajiri wa Maduka ya Vunjabei nchini Tanzania, Fred Fabian Ngajiro almaarufu Fred Vunjabei, anadaiwa kuwavuruga kabisa mastaa wa kike Bongo, RISASI JUMAMOSI limedokezwa.


Jina la Fred Vunjabei limeendelea ‘kutrendi’ kwenye mitandao ya kijamii akihusishwa kutoka kimapenzi na warembo mastaa kibao Bongo.

 

LISTI NI NDEFU


Gazeti hili limechimba undani wa skendo hiyo na kuibuka na listi ndefu ya warembo wanaodaiwa kutibuana wenyewe kwa wenyewe ambapo uchunguzi ulipofanyika, ilibainika kwamba chanzo cha yote ni ukaribu wa wahusika hao na Fred Vunjabei.

 

Fred Vunjabei mwenye umri wa miaka 33 ni mjasiriamali wa kisasa ambaye ni mfanyabiashara wa mtandao wa maduka ya mavazi ya Vunjabei ambayo inasemekana yamechangia kwa kiasi kikubwa yeye kuwa na ukaribu na mastaa hao.

 

Pia anatajwa kumiliki lebo ya muziki ya Too Much Money inayowasimamia wasanii mbalimbali wa Bongo Fleva wakiongozwa na msanii mkali kutoka Arusha, Oscar John Lelo ‘Whozu’.

 

Baadhi ya warembo wakali wa mjini wanaotajwa kwenye listi ya skendo hiyo ni pamoja na mwanamitindo na msanii Hamisa Mobeto, ma-video vixen Nairati Ramadhan ‘Official Nai’ na Anna Kimario Sebastian ‘Tunda’.


Wengine ni wasanii wa kike wa Bongo Fleva, Lulu Abbas ‘Lulu Diva’, Lulu Euggen ‘Amber Lulu’ na Gift Stanford ‘Gigy Money’.

 

Pia wanatajwatajwa waigizaji wa Bongo Movies kama Wema Isaac Sepetu, Jacqueline Wolper Massawe na Kaitesy Abdul ‘Tessy Chocolate’ ambaye ni mzazi mwenza wa msanii mkubwa wa Bongo Fleva, Aslay Isihaka.

 

FRED VUNJABEI NA MOBETO


Miongoni mwa habari zilizoteka hisia za wengi kwenye mitandao ya kijamii mwaka 2020 ni tetesi za Fred Vunjabei kutoka kimapenzi na mwanamama Mobeto ambaye ni baby mama wa staa wa muziki barani Afrika, Nasibu Abdul ‘Diamond Platnumz’ na Mtendaji Mkuu wa Kampuni ya EFM Limited, Francis Antony Ciza ‘DJ Majizo’.

 

Kwa mujibu wa tetesi hizo, Fred Vunjabei amekuwa na ukaribu wenye viulizo vingi na Mobeto, kiasi cha wote wawili kujitokeza hadharani na kukanusha si wapenzi.

 

Hata hivyo, mbali na kudaiwa kumnunulia Mobeto lile ndinga aina ya Toyota Prado, mapema wiki hii yameibuka mengine mazito.

 

Mobeto ametamba kufunguliwa duka jipya la nguo za watoto liitwalo Kids Coner akimshukuru mpenzi wake ambaye hakumtaja kwa kumfungulia duka hilo la mtaji mkubwa.

 

Kama kawaida, wananzengo wameunganisha doti na kudai kuwa, duka hilo, Mobeto amefunguliwa na Fred Vunjabei ambapo amefanya yote hayo wakati mrembo huyo akiwa nchini Nigeria.

 

Katika utetezi wake juu ya kuwa na uhusiano wa kimapenzi na Mobeto, Fred Vunjabei anasema;


“Ukiwataja marafiki zangu utaanza na Mobeto kisha utamalizia kwa Frank Knows.


“Sina uhusiano na Hamisa (Mobeto) zaidi ya urafiki wa kawaida na kikazi na ushauri, sijamuajiri kwa sababu siwezi kumuajiri, lakini ni mtu tunayeshauriana katika mambo mengi ya msingi.”

 

…NA TESSY


Fred Vunjabei pia anatajwa na Tessy Chocolate, ikisemekana kwamba, waliwahi kuwa kwenye uhusiano wa kimapenzi ambapo wakati wa penzi lao walikuwa wakitaradadi pamoja kila sehemu hasa kwenye viwanja vya bata ndefu ambapo walikuwa wakila bata hadi kuku wanaona gere.

 

Madai hayo yalikwenda mbali zaidi na kusemekana kwamba, hata ile saluni ya Tessy maeneo ya Sinza jijini Dar ambayo ilisababisha akavamiwa, ilikuwa na mkono wa jamaa huyo.

 

Akizungumzia uhusiano wake wa Tessy, Fred Vunjabei anasema;


“Tessy ni mwanangu sana, ni mshikaji wangu na najua ana mpenzi wake.”

 

…NA NAI


Mbali na hao, pia Fred Vunjabei anatajwa kutoka kimapenzi na video vixen Official Nai, kiasi cha kujikuta akiingia kwenye bifu zito na mwenzake, Gigy Money.

 

Nai na Gigy wamekuwa kwenye bifu kali mno ambapo kwa mujibu wa watu wao wa karibu, Fred Vunjabei ndiye chanzo baada ya warembo hao kutuhumiana kuchukuliana danga lao hilo.

 

Kuhusu kutoka kimapenzi na Nai, Fred Vunjabei anasema;


“Mimi nimemfahamu Nai tangu akiwa kidato cha pili, ni kweli Nai ni pisi kali na ananicheki mara kwa mara, kama ningekuwa na mambo hayo (mapenzi) ningefanya zamani. Nai ni mshikaji tu.”

 

…NA GIGY


Pia Fred Vunjabei amekuwa akitajwa na Gigy Money ambapo kuhusu mrembo huyo anajitetea; “Hakuna kitu kama hicho.”

 

…NA AMBER LULU


Kumekuwa na ugomvi mzito kati ya Amber Lulu, Gigy Money na Nai ambapo wote kwa pamoja inasemekana unatokana na kila mmoja kumtuhumu mwenzake kumuingilia kwa Fred Vunjabei.


…NA TUNDA MAHOTELI


Kwenye orodha hiyo anatajwa pia video vixen Tunda almaarufu Tunda Mahoteli ambaye anadaiwa kufunguliwa duka na Fred Vunjabei kutokana na uhusiano wao wa kimapenzi.


Hata hivyo, katika utetezi wake, Fred Vunjabei anasema;

 

“Tunda yupo chini ya Lebo ya Too Much Money. Amejiingiza kwenye biashara ya nguo hivyo tunamlea ili kuona anakuwa kidogokidogo kibiashara na si kingine.


“Tunatafuta namna ya kumsapoti kwa namna moja au nyingine ili nay eye akue kwenye eneo la biashara.


“Duka ni la Tunda hata kama akiwaonesha TIN namba, duka ni la kwake. Ninachokifanya ni kumuonesha njia ili akue.”

…NA WEMA


Kabla ya wote hao, unakumbuka lile duka la ngo za watoto la Wema? Basi fahamu kwamba, Fred Vunjabei pia alihusishwa, lakini kila mmoja alikanusha jambo hilo.

FRED VUNJABEI AFUNGUKA KWA JUMLA

Akifunguka kwa jumla juu ya yeye kuhusishwa kimapenzi na warembo kibao Bongo, Fred Vunjabei anasema;


“Mimi nikikaa nao (mastaa) huwa tunazungumzia mambo ya biashara, hatujawahi kuzungumza kuhusu mambo yaliyo nje ya hayo.”


FRED VUNJABEI NI NANI?


Fred Vunjabei ni Mkurugenzi Mkuu na Mwanzilishi wa Kampuni ya Vunjabei (T) Group Limited. Pia ndiye Mwanzilishi na Rais wa Lebo ya Too Much Money Limited.


Fred Vunjabei anatajwa kuwa mmoja wa wafanyabiashara wenye umri mdogo na mafanikio makubwa nchini Tanzania. Fred Vunjabei amehitimu shahada ya biashara mwaka 2010 katika Chuo Kikuu cha Dar (UDSM).

Pia ana shahada ya juu ya usimamizi wa biashara kutoka Chuo Kikuu cha Mzumbe. Mara tu baada ya kufuzu masomo yake ya chuo kikuu mwaka 2014, Fred Vunjabei aliamua kujiajiri kwa kuanza biashara ndogondogo na kwa mtaji mdogo.


Mwaka 2015 alisafiri kwenda China ili kutafiti juu ya fursa za kibiashara na ndipo alipogundua kuwa kuna fursa kubwa upande wa mavazi na urembo.


Alirudi nchini Tanzania na kuanzisha kampuni iitwayo Vunjabei (T) Group Limited na kufungua duka lake la kwanza Kariako jijini Dar ambalo lilifanya vizuri na kuweza kuwekeza katika kufungua maduka mengine katika mikoa mbalimbali ya Tanzania.


Licha ya kuwa na maduka mengi ya nguo katika mikoa mbalimbali Tanzania, pia alianzisha kampuni ya usimamizi wa vipaji vya muziki Tanzania inayoitwa Too Much Money Limited.


Fred Vunjabei anatajwa na jarida moja nchini kama mmoja wa mamilionea wenye umri mdogo Tanzania.