Spika wa Bunge Job Ndugai, amewaapisha Dkt Dorothy Gwajima na Dkt Leonard Chamuriho kuwa Wabunge wa Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.

Wabunge hao wameapishwa kufuatia kuteuliwa na Rais John Magufuli hivi karibuni na kisha kupewa nyadhifa za Uwaziri katika Baraza jipya la Mawaziri alilolitangaza.

Hafla ya kuwaapisha Wabunge hao wawili imefanyika jijini Dodoma na kuhudhuriwa na watu mbalimbali.

Dkt Dorothy Gwajima ambaye alikuwa Naibu Katibu Mkuu Ofisi ya Rais Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (TAMISEMI) anayeshughulikia Afya ameteuliwa kuwa Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto.

Dkt Leonard Chamuriho aliyekuwa Katibu Mkuu wa Wizara ya Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano anayeshughulikia Uchukuzi ameteuliwa na Rais Magufuli kuwa Waziri wa Ujenzi na Uchukuzi.