Na Shamimu Nyaki – WHUSM, Dar es Salaam
Waziri wa Habari, Utamaduni Sanaa na Michezo Mhe. Innocent Bashugwa amempongeza Mshindi wa Urembo Tanzania (Miss Tanzania) kwa mwaka 2020, Bi. Rose Manfere kwa kutwaa taji hilo ambapo amemtaka kutumia urembo wake kuitangaza nchi vizuri.

Mhe. Bashungwa ametoa pongezi hizo jana Desemba 19, 2020 Jijini Dar es Salaam alipokutana na Mrembo huyo ambapo ameahidi kuwa Serikali itaendelea kumpa ushirikiano katika kutekeleza wajibu wake kwa Taifa kwa kuwa kwa sasa amebeba dhamana ya kutangaza nchi kwenye tasnia hiyo.

“Serikali tutakuunga mkono katika jukumu hili ulilopata la kupeperusha Bendera ya nchi katika tasnia ya urembo kwa mwaka mmoja, nasisitiza tumia firsa hii kutangaza utamaduni wetu, mila na desturi za taifa letu na zaidi utalii unaopatikana hapa nchini”alisema Mhe.Bashungwa.

Aidha Mhe.Bashungwa amempongeza Mratibu wa Mashindano hayo Bi.Basilisa Mwanukuzi kwa kuendesha mashindano hayo kwa weledi ambayo yamefanikisha kupatikana kwa mwakilishi wa kutangaza nchi na katika mashindano ya Urembo ya Dunia yanayotarajiwa kufanyika mwaka 2021.

Naye Mratibu wa Mashindano hayo Bi. Basilisa Mwanukuzi ameishukuru Serikali kwa kutoa mchango mkubwa katika kufanikisha mashindano hayo ambapo ameahidi kuwa Mrembo huyo atafanya vizuri katika mashindano ya Dunia.

“Watanzania naomba tutoe ushirikiano kwa Mrembo huyu katika kazi yake ya kuitangaza nchi yetu kupindia urembo, akifanikiwa nchi pia imefanikiwa hivyo tumuunge mkono” alisema Bi Basilisa.

Mashindano hayo yamefanyika yamefanyika hivi karibuni Jijini Dar es Slaam.