BAADA ya kukithiri kwa madai ya wananchi na kuongezeka kwa mijadala kwenye mitandao ya kijamii, kufuatia  kilio cha wananchi wakidai kutapeliwa na kampuni  ya QNET  mkoani Kilimanjaro, Jeshi la Polisi limeamua kuingilia kati.

Kila kona sasa ni kilio cha wananchi kutapeliwa mamilioni ya fedha,  ambapo wapo waliofikia hatua hata ya kuacha kazi, hasa watumishi wa umma kwa ahadi tamutamu za kuvuna fedha kutoka kampuni ya biashara za mtandao ya QNET.

Mkurugenzi wa Upelelezi wa Makosa ya Jinai wa Jeshi la Polisi, Robert Boaz alisema jeshi hilo limeanzisha uchunguzi kwa kampuni ya QNET baada ya kupokea malalamiko mengi ya watu kutapeliwa na kampuni hiyo.

“Tumeshapokea malalamiko mengi, kuna uchunguzi tunaufanya kuhusu QNET jinsi wanavyofanya shughuli zao,” alisema Boaz huku akitahadharisha wananchi kuepuka biashara za upatu.

“Basically (kimsingi), Pyramid scheme (upatu) ni kosa la jinai, kwa sababu mnapoanza mnakuwa wachache na mnaweza mkalipana kidogo kwa kuchangiana kama mko wawili watatu na kama sharti mlipwe na waliochini, maana yake mtalipana na mkatoana.


“Lakini kadiri idadi inavyokuwa kubwa ndivyo inavyokuwa vigumu kulipana, kwa hiyo kuna watu ambao hatalipwa. Kwa msingi huo kitendo hicho kiliharamishwa kwa mujibu wa sheria” alisema Kamishna Boaz.