BODI ya Wakurugenzi ya Simba inakutana kwa haraka kujadili adhabu ya faini ya Sh 294 milioni ambazo Shirikisho la Soka Duniani, Fifa kupitia kitengo cha usuluhishi cha migogoro ya soka imetaka kulipa kwa kukiuka taratibu za kumsajili Shiza Kichuya, lakini wamemtaja Senzo Mazingisa kwenye ishu nzima.
Kichuya alisajili akitokea Pharco FC ya Misri wakati huo Senzo akiwa Ofisa Mtendaji Mkuu kabla ya kuhamia Yanga.
Simba imetakiwa kulipa fedha hizo au kuingia kwenye adhabu ya kutosajili kwa misimu miwili endapo itashindwa kulipa pesa hizo ndani ya siku 45 kuanzia Novemba 24, mwaka huu, ilipotolewa hukumu hiyo.
Simba ilimuuza Kichuya Januari, mwaka jana kwa mkataba wa miaka minne kwenye klabu ya Pharco ya Ligi Daraja la Pili kabla ya mabosi wake kumpeleka kwa mkopo ENPPI ya Ligi Kuu ya.
ENPPI ilimtumia kwa muda wa miezi sita tu na kumrejesha Pharco mwanzoni mwa mwaka huu ambako, hakupata nafasi ya kucheza na klabu kupanga kumpeleka kwingine kwa mkopo, jambo ambalo Kichuya ni kama hakukubaliana nalo na kuamua kurejea nchini na kusajiliwa na Simba bila ridhaa Pharco aliokuwa na mkataba nao.
Fifa imemfungia mchezaji huyo kucheza soka kwa miezi sita huku Simba wakipigwa faini ya dola 127,000 za Marekani (Sh 294 Milioni).
Kwa nyakati tofauti jana, viongozi wenye ushawishi ndani ya klabu ya Simba, Salim Abdallah ‘Try Again’ na Mulamu Mghambi, walisema hawajui kitu gani kimetokea, ingawa mwenye ukweli kuhusu suala lote ni Senzo.
“Sina maelezo ya kutosha kwenye suala hili, ila nijuavyo tuliomba ITC tukapewa, kipindi ambacho yupo Senzo, sijui nini kimetokea,” alisema Mulamu kauli sawa na iliyotolewa na Try Again.
Alisema wakati wa usajili wa Kichuya, Senzo ndiye aliyekuwepo, hivyo ana nafasi nzuri ya kulizungumzia sakata hilo, ingawa wachambuzi wa soka wamedai anasingiziwa kwa kuwa, mtu anayehusika na uhamisho ni Meneja wa TMS, ambaye angebaini kama kulikuwa na dosari.
Hata hivyo, walisema watalijadili suala hilo litakapoletwa na Mtendaji Mkuu wao, Barbara Gonzalez.
“Sijui tutakutana lini maana ni hivi karibuni tumetoka kwenye kikao, lakini tutakapokuta CEO atalileta mezani, tutalijadili na kujua nini tufanye,” alisema Mulamu.
Mwanaspoti lilijaribu kumsaka Senzom kwa njia ya simu, ila hakupatikana na hata alipotumiwa ujumbe mfupi aliusoma bila kujibu, huku ikielezwa yupo safarini na kikosi cha Yanga.
Kikosi cha Yanga jana kilisafiri kwenda Mwanza kabla ya kujisogeza Shinyanga kwa ajili ya mechi yao ya Ligi Kuu Bara dhidi ya Mwadui inayopigwa kesho Uwanja wa Kambarage.
NA IMANI MAKONGORO