Rais Dkt. John Magufuli amewaagiza Mawaziri na Naibu Mawaziri aliowateua na kuwaapisha kufanya maamuzi yenye maslahi kwa Taifa.

Akizungumza mara baada ya kuwaapisha Mawaziri 21 na Naibu Mawaziri 22 Ikulu Chamwino jijini Dodoma, Rais Magufuli amesema kuwa ni bora kufanya uamuzi mbaya kuliko kutofanya uamuzi kabisa.

“Ni nafuu kufanya uamuzi mbaya kuliko kutofanya uamuzi, kwa sababu tatizo letu lingine tulilonalo unashindwa kutoa uamuzi kwa sababu hutaki uonekane mbaya uwe neutral neutral sasa sifahamu utafanya uamuzi lini, kafanyeni uamuzi hasa unaohusu maslahi ya Taifa” amesisitiza Rais Magufuli.

Pia amewataka Mawaziri na Naibu Mawaziri hao kushirikiana, na Mawaziri kwa kutambua Naibu Mawaziri ni wasaidizi wao hivyo wawapangie kazi.

Disemba 5 mwaka huu Rais Magufuli aliwateua Mawaziri 21 na Naibu Mawaziri 23 kuingia kwenye Baraza jipya la Mawaziri lenye Mawaziri 23 na Naibu Mawaziri hao 23.