Wakili wa kujitegemea, Profesa Abdallah Safari ameishauri Chadema kwenda mahakamani kuomba tafsiri ya uhalali wa ubunge wa makada 19 wa chama hicho walioadhibiwa baada ya kwenda kuapa kuwa wabunge wa viti maalum na kutotokea mbele ya Kamati Kuu kujieleza.


Wanachama hao, ambao ni pamoja na mwenyekiti wa Baraza la Wanawake (Bawacha), Halima Mdee waliapishwa Novemba 24 wakati kukiwa na utata wa barua iliyopelekwa Tume ya Uchaguzi (NEC) kuhusu uteuzi wa wabunge wa viti maalum, baada ya katibu mkuu wa Chadema, John Mnyika kusema hakuiandika wala Kamati Kuu haikukutana kupitisha orodha.Kitendo hicho kiliifanya Chadema iwate mbele ya Kamati Kuu kujielezas, lakini wote hawakutokea na hivyo chombo hicho kufikia hatua ya kuwavua uanachama, lakini Spika Job Ndugai alisema hatatambua uamuzi huo aliodai wa kuonea wanawake baada ya kuhukumiwa bila ya kusikilizwa.Nafasi za viti maalum ni za vyama ambavyo hupata zaidi ya asilimia tano ya kura za wabunge, tofauti na za ubunge wa jimbo ambazo hupatikana kutokana na vyama humdhamini mgombea.“Kama wataenda bungeni, njia pekee ni kuomba tafsiri ya mahakama ili chombo hiki kiseme katika mazingira haya ibara ya 71 (1) f hawa ni wanachama halali,” alisema Profesa Safari, ambaye amebobea katika sheria.Ibara hiyo ya katiba inasema mtu atapoteza ubunge iwapo “ataacha kuwa mwanachama wa chama alichokuwamo wakati alipochaguliwa au alipoteuliwa kuwa mbunge”.Profesa Safari, aliyewahi kuwa makamu mwenyekiti wa Chadema kuanzia 2014 hadi 2019, alisema kuna haja ya kufungua kesi kupata tafsiri kama Mdee na wenzake bado ni wabunge halali baada ya Kamati Kuu ya Chadema kuwavua uanachama.“Mahakama ndiyo ina haki ya kutafsiri,” alisema.Profesa Safari alisema suala la Mdee na wenzake kufukuzwa Chadema lipo wazi kwa mujibu wa ibara ya 71 (1) (f) ya Katiba ya jamhuri ya Muungano inayoeleza kuhusu mbunge kufukuzwa uanachama na pia sifa za kugombea zinazoelezwa katika ibara 67 (1)b, inayotaka mgombea ubunge apendekezwe na chama chake.“Dhana ya kuwa na chama ni muhimu. Ukishatimuliwa huwezi ukakingikiwa kifua na mtu yeyote. Bahati nzuri matukio yametokea mara nyingi sana. Wakati wa Tanu walifukuzwa kina Anangisye, halafu wabunge wa CUF walitimuliwa. Mara nyingi tu (haya yanatokea),” alisema Safari.Pia alielezwa kushangazwa na kitendo cha Spika kuwatetea makada hao akihoji wameanza urafiki lini.“Halima na (Esta) Bulaya walishafukuzwa na kukaa nje ya Bunge kwa mwaka mmoja,” alisema.‘‘Kwa nini leo anakuwa na nguvu ya kuwakingia kifua kinyume na Katiba? Pamoja na mazoea ya vyama, hapo awali alishawafukuza. Kuna kitu hawa hawataki kukisema, lakini kuna siku watakisema.”Hata hivyo, Profesa Safari alisema hataki kuingia kwa undani kuzungumzia suala hilo, lakini muda utaongea.Alisema kama Mdee na wenzake wanampinga mwenyekiti, nini maana ya kwenda bungeni.“Kamati Kuu ilishasema kuwa haiwezekani na imeshatoa maelekezo, lakini kuna watu wanauliza mbona yule mbunge mwingine (Aida Kenan-Nkasi) anaachiwa? Kamati Kuu ilikuwa ajenda yake ya kina Halima. Yule atashughulikiwa ikifika muda,” alisema Profesa Safari.Kamati Kuu ilishafikia uamuzi kama huo kwa mbunge wa zamani wa Kigoma Kaskazini, Zitto Kabwe, lakini alifungua kesi mahakamani na kuzuia vyombo vya chama hicho kujadili suala lake hadi kesi hiyo ilipoisha kwa kiongozi huyo wa ACT-Wazalendo kwa sasa kushindwa.Katika Bunge lililopita, Chadema iliwavua uanachama wabunge wake wanne, Joseph Selasini (Rombo), Anthony Komu (Moshi Vijijini), David Silinde (Momba) na Wilfred Lwakatare (Bukoba Mjini) kwa kukiuka maagizo ya chama.Hata hivyo, wabunge hao waliendelea na vikao mpaka ukomo wa Bunge hilo.Julai 26, 2017, Spika Ndugai baada ya kujiridhisha kwamba wabunge wanane wa CUF walitimuliwa, alitangaza kuwa nafasi zao ziko wazi na kuiandikia NEC iendelee na hatua za kujaza nafasi hizo.Mbali na Mdee, wanachama wengine waliovuliwa uanachama ni wengine ni Ester Bulaya, Ester Matiko, Agnesta Lambert, Grace Tendega, Salome Makamba, Jesca Kishoa , Tunza Malapo na Conchestar Rwamlaza, Naghenjwa Kaboyoka. Hawa Mwaifunga, Stella Fiao, Anatropia Theonest, Asia Mohammed, Sophia Mwakagenda, Nusrat Hanje, Cecilia Pareso na Felister Njau.Katika moto wa kutoa nafasi sawa kwa wanawake, ibara ya 66 (1)(e) ya Katiba ya jamhuri ya Muungano inasema wabunge wanawake wanatakiwa kuwa si chini ya asilimia 30 na sifa zao, ikiwa ni pamoja na wale wanaoteuliwa na vyama vyao vya siasa kwa uwiano wa kura za ubunge.