Waziri Mkuu Mstaafu Mizengo Pinda ametoa wito kwa taasisi za kifedha ikiwemo mabenki kuweka masharti nafuu na riba kidogo ili kuwafanya vijana wengi wakope na kuanzisha shughuli za kilimo.

Ametoa wito huo jana (03 .12.2020) jijini Dodoma wakati akifungua Mkutano Mkuu wa mwaka wa Wadau wa Sekta ya Kilimo ulioandaliwa na Jukwaa Huru la Wadau wa Kilimo (ANSAF) na kushirikisha zaidi ya mashirika 84 yasiyo ya kiserikali na wawakilisha iwa wakulima.

“Taasisi za kifedha zimeweka masharti mengi ambayo hayavutii vijana kukopa ili wajiendeleze katika sekta ya kilimo,” alisema na kuo wito kwa mabenki kupitia upya sera zao za  mikopo ili kilimo kiajili vijana wengi tofauti na sasa.

Waziri Mkuu huyo Mstaafu Pinda amebainisha kuwa yeye mwenyewe ni mkulima kwa vitendo ambapo amesema bila upatikanaji wa mikopo yenye masharti nafuu itakuwa vigumu kwa vijana kujiajili kupitia kilimo.

Aliongeza kusema anaipongeza Serikali ya Awamu ya Tano kwa kusambaza umeme kwenye vijiji vingi nchini hali inayosaidia vijana na wananchi wengi kufanya shughuli za ujasiliamali ikiwemo kilimo cha mboga mboga na matunda.

Pinda amezitaka wizara za Kilimo, Mifugo na Uvuvi na ile ya Viwanda na Biashara kuhakikisha zinatengeneza mazingira wezeshi ya uanzishwaji viwanda vidogo ili viajili vijana wengi na kutumia malighafi zitokanazo na sekta ya kilimo.

Akiongea kuhusu takwimu za ajira kwenye kilimo, Pinda alisema sekta ya kilimo imeajili  asilimia 65 ya watanzania huku sekta ya huduma ikiwa na asilimia 28 na sekta ya viwanda imeajili asilimia 07 pekee. Amesema ili uchumi wa viwanda uweze kukua kwa kasi ni budi sekta ya kilimo ikapewa kipaumbele zaidi.

“Tuhakikishe tunasindika mazao yetu ya kilimo, mifugo na uvuvi ikiwemo nyuki ili viwanda vyetu hasa vidogo vipate malighafi na kuwezesha ajira nyingi kuzalishwa hapa hapa nchini badala ya kuuza mazao ghafi ,hivyo wizara ziendeleze jitihada za kuanzisha viwanda vingi vidogo” alisema Waziri Mkuu Mstaafu Pinda.

Kwa upande wake Katibu Mkuu Wizara ya Kilimo Gerald Kusaya amesema ili kuwezesha vijana wengi kushiriki katika kilimo serikali imenzisha mkakati wa kuhamasisha wakulima kupima afya ya udongo ili kujua tabia yake hali itakayokuza tija na uzalishaji wa mazao ya kilimo.

Kusaya alibainisha kuwa wizara ya kilimo kwa kutumia Kituo cha Utafiti wa Kilimo (TARI) Selian cha Arusha inakusanya sampuli za udongo toka kwenye kata zote 3,956 nchini ili zipimwe na kujua tabia yake ili hatimaye itengenezwe ramani inayoonesha tabia za udongo kwa nchi nzima.

“Tayari tumefanikiwa kukusanya sampuli za udongo 30,400 kutoka kwenye mikoa 18 ya Tanzania bara ili tupime tabia yake na kuwajulisha wakulima aina ya mazao ya kupanda na aina gani ya mbolea kutumia kwenye udongo huo ili kukuza tija na uzalishaji wa mazao” alisema Kusaya

Katibu  Mkuu huyo wa Kilimo alisema kupitia jitihada hizo vijana watavutika kuanzisha shughuli za kilimo kwani watakuwa na uhakika wa kilimo cha kibiashara endapo watajua tabia ya udongo na aina gani ya mbolea itakayotumika na kuepuka kufanya kilimo cha kubahatisha.

“Tutawafundisha vijana umuhimu wa kupima afya ya udongo ili wajue aina ya mazao  na mbolea ya kutumia kwenye maeneo yao huko huko vijijini kupitia mkakati huu wa wizara “ alisisitiza Kusaya.

Kwa upande wake Mkurugenzi Mkuu wa ANSAF Audax Rukonge akizungumza kwenye kongamano hilo alisema watajadili namna ya uongeza wigo wa vijana kushiriki kwenye kilimo kwai takwimu zinaonesha ni asilimia 10 tu ya vijana wanaohitimu shule na vyo nchini wanajihusisha na kilimo.

“Kati ya vijana 800,000 hadi 1,000,000 wanaohitimu shule na vyuo nchini Tanzania kwa mwaka ni asilimia 10 pekee wameajiliwa au kujiajili kwenye sekta ya kilimo hali inayofanya wengi kutegemea sekta zingine kuajiliwa  na kuwa tunalo jukumu la kuwaandaa vijana watambue fursa kwenye kilimo” alisema Rukonge.

Rukonge aliongeza kuwa ANSAF kwa ushirikiano na mashirika wenza kufuatia kuona fursa  zipo kwenye kilimo imekuwa ikiandaa kongamano la kila mwaka kujadili upatikanaji wa mazingira wezeshi kwa vijana wengi kujiajili kwenye kilimo nchini ambapo kongamano hili linafanyika kwa mara ya 13 sasa.