SIKU chache zilizopita kuliibuka gumzo mitandaoni baada ya picha za baba mzazi wa mwanamuziki mkubwa barani Afrika, Nasibu Abdul ‘Diamond Platnumz’, Abdul Isaack Jumaa ‘Mzee Abdul’ kusambaa akionekana akigombea daladala.

 

Habari za ndani ya familia ya Diamond au Mondi zinaeleza kwamba, picha hizo zimeivuruga vilivyo familia hiyo.

 

DALADALA LA MBURAHATI-MNAZI MMOJA

Awali, kurasa mbalimbali za udaku mtandaoni zilianza kuposti picha hizo zikimuonesha mzee huyo akiwa amebeba mfuko wa salfeti begani huku akigombea kuingia ndani ya gari hilo la abiria (dalada) linalofanya safari zake kati ya Mburahati na Mnazi-Mmoja jijini Dar.



HATA BAJAJ?

Jambo hilo lilisababisha huzuni kubwa kwa baadhi ya mashabiki, wakihoji ni kwa nini Mondi anashindwa kumnunulia baba yake hata Bajaj ya kutembelea?

 

“Jamani hivi Simba (Mondi) huyu ni baba yake mzazi kweli? Maana ninavyojua huwezi kumuacha baba yako akapata shida kiasi hiki, mzee anapigwa na jua, utadhani mtoto hana pesa, hii siyo sawa kabisa, dogo (Mondi) anatakiwa abadilike,” aliandika shabiki mmoja aliyefahamika kwa jina la Mike.

 

“Sidhani kama Chibu (Mondi) anajali, maana angekuwa anamjali angemhudumia baba yake, watu tuna hukumu tu ila laiti wazee wao wangewakana kama huyu mzee wasingemtukana Mondi,” aliongeza Ot Lingerie.

 

“Diamond mtengenezee maisha mazuri huyo mzee, usiangalie ya zamani, inauma sana, fungua hata biashara yoyote mpe asimamie, utapata thawabu kubwa kutoka kwa Mwenyezi Mungu,” aliandika Maneke Vincent.

Hayo ni baadhi ya maoni ya wananzengo huko mtandaoni ambapo kila mmoja alikuwa akizungumza la kwake.



HATUA ZA KISHERIA

Hata hivyo, wakati mambo yakiendelea kupamba moto, ghafla ziliibuka tetesi kwamba tayari uongozi wa Wasafi Classic Baby (WCB) iliyo chini ya Mondi umeingia kazini kumsaka mtu aliyesambaza picha hizo kwa lengo la kumchukulia hatua za kisheria kwani huo ni udhalilishaji.

 

“Hivi tunavyoongea nimesikia kwamba uongozi wa WCB umeshaingia kazini kumsaka huyo mtu aliyesambaza hizo picha ili sheria ichukue mkondo wake maana ni kama wanamuaibisha msanii wao,” alisema mtu wa karibu wa Wasafi akisisitiza kwamba, ishu hiyo imeibua tafrani mno ndani ya familia hiyo.

 

MONDI ANASEMAJE?

Gazeti la IJUMAA WIKIENDA lilifanya jitihada za kumtafuta Mondi ili kujua msimamo wake kuhusu hatma ya baba yake, lakini kwa bahati mbaya simu yake iliita bila kupokelewa na hata alipotumiwa chatting kwenye WhatsApp zilionesha kumfikia, lakini hakujibu.

 

DARLEEN SASA

Kutokana na hali hiyo, Gazeti la IJUMAA WIKIENDA lilimgeukia dada wa msanii huyo, Mwanahawa Abdul ‘Queen Darleen’ ambaye kwa upande wake alipoulizwa swali hilo la ni kwa nini wanashindwa kumhudumia baba yao ilihali wao wana maisha mazuri huku baba akidhalilika kiasi kile, alijibu kwa ukali na kukata simu.

 

“Wewe pia si una baba? Basi achana na maisha ya watu,” Darleen alimjibu mwandishi wetu na kukata simu.

 

MENEJA ANASEMAJE?

Gazeti la IJUMAA WIKIENDA haikuishia hapo kwani lilimtafuta mmoja wa mameneja wa Mondi, Said Fella ‘Mkubwa Fella’ ambapo kwa upande wake alisema kuwa, mambo hayo ni ya kifamilia hivyo anatakiwa aulizwe Mondi mwenyewe.

 

“Nimeziona hizo picha, lakini mimi siwezi kusema lolote, yaani mkitaka niongee mtakuwa mnanionea, kwa sababu hayo ni mambo ya kifamilia zaidi, hebu mtafuteni Nasibu (Mondi) mwenyewe ndiyo atajibu vizuri maswali yenu,” alisema Mkubwa Fella.