Ofisa ugavi wa Halmashauri ya Manispaa ya Moshi, Dominic Mwapombe amekamatwa kwa agizo la Mkuu wa Wilaya ya Hai, Lengai Ole Sabaya akidaiwa kuwa miongoni mwa viongozi wa kampuni moja (jina tunalo) inayotuhumiwa kutapeli watumishi wa Serikali.


Mwapombe anadaiwa kuwashawishi walimu na wastaafu kujisajili na kampuni hiyo ambayo inadaiwa haijasajiliwa na Wakala wa Usajili wa Biashara na Leseni (Brela).


Sabaya alisema hayo jana katika mkutano wa wakuu wa shule ulioihusisha kamati ya usalama ya wilaya baada ya walimu na baadhi ya wafanyabiashara kuanika madai ya utapeli wa kampuni hiyo.
Mkuu huyo wa wilaya alidai mtumishi huyo amekuwa akiwashawishi watumishi wa Serikali kutoa Sh4.3 milioni kama kiingilio cha kujiunga na kampuni hiyo, huku walengwa wakiwa ni walimu, manesi, madaktari, wastaafu pamoja na wafanyabiashara.
Wakati wakieleza hayo, Mwapombe alikuwepo katika mkutano huo na Sabaya kuagiza akamatwe akitaka Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (Takukuru) na polisi kumbana ili awaonyeshe walipoziweka fedha wanazodaiwa kutapeli na kuutaja mtandao wao.

“Walimu hawa wamedhulumiwa, wametapeliwa fedha zao, familia haziko sawa watu wamefarakana kwa sababu ya hii kampuni. OCD na Takukuru mkamateni huyu mtu awapeleke kwa watu wote aliochukua fedha zao kwenye yale matawi yao mpaka tupate mtu wa mwisho.”

“Watu wote waliodhulumiwa fedha zao na hii kampuni wilaya hii waje hapa.... hawa watuambie wanarudishaje fedha za watu na lazima waseme watu wake wote ambao wako naye,” alisema Sabaya.

Aliongeza kuwa kampuni hiyo imekuwa ikichukua fedha za watu wakiwamo wajane na imesababisha ndoa za watu kuvunjika, wengine wameuza mashamba na wengine wamelazwa hospitali kwa magonjwa ya moyo.

“Kama hiyo fedha ingekuwa na raha na rahisi kiasi hicho haya mabenki yetu yasingefanya hiyo biashara, wiki mbili zilizopita kuna mwalimu wetu hapa Hai kadhulumiwa fedha zake na tumemrudishia Sh4.2milioni.”

“Hii kampuni haijasajiliwa Brela wala jina la hii kampuni halipo kabisa huko. Nyinyi ni wababaishaji tunajua mnachokifanya, walengwa wenu ni hawa walimu wetu, manesi, madaktari, wastaafu na wafanyabiashara,” alisema Sabaya

Katika mkutano huo, Sabaya alimpigia simu Mkurugenzi Mkuu wa Brela, David Nyaisa na kuweka sauti ili kila mmoja asikilize akihoji kama kampuni hiyo imesajiliwa ama la.

Nyais alijibu akisema; ‘‘ Siifahamu na haijasajiliwa hapa kwetu, tumekuwa tukiulizwa na taasisi mbalimbali za Serikali na tumewajibu kwa maandishi kwamba haipo hapa Brela.’’

Kabla ya kutiwa mbaroni, Mwapombe alijitetea na kusema kuwa kampuni hiyo ina vibali vyote vikiwamo vya Brela na Mamlaka ya Dawa na Vifaa Tiba (TMDA) na kwamba ni kampuni inayofanya biashara za kifedha na sio kutoa mikopo.

“Hii siyo kampuni ya kutoa mikopo ni kampuni ya biashara ya kifedha mtandaoni, maelezo ya kina anaweza kutoa wakala mkuu ila mimi najua vipo vyeti vinavyoitambua hii biashara,” alisema.

Wakizungumza katika kikao hicho baadhi ya wananchi walisema watu hao huwafuata na kuwahakikishia kuwa kampuni imesajiliwa Brela na kwamba kiwango cha kujiunga ni Sh4.3 milioni.

Janeth Julius, mkazi wa Moshi alisema watendaji wa ka kampuni hiyo walimfuata na kumpa uhakika wa fedha zake na kwamba kati ya Sh4.3 milioni ambayo angeitoa kila mwezi angewekewa dola 200 kwenye akaunti yake jambo ambalo sio kweli na mpaka sasa hajawahi kuona fedha hizo tangu ajiunge mwaka 2019.

“Nilitoa Sh4.3 milioni ambapo nilipewa saa ya mkononi na wakaniambia kila mwezi wataniingizia dola 200 kwenye akaunti yangu kwamba nitafute wenzangu watatu au wanne nikawaambia sawa, lakini wakati huo natoa fedha hizi taslimu mkononi sikupewa risiti.”


“Baadaye kidogo niliwaomba risiti wakaniambia iko kwenye mtandao..., cha kushangaza mpaka sasa sijaona hizo fedha nilizoambiwa niko kwenye wakati mgumu..., ndoa yangu iko matatani sina ndoa na hizi fedha nilizotoa nilikopa naomba msaada wako mkuu. Nisaidie sijui nitafanya nini mimi,” alieleza kwa uchungu huku akibubujikwa na machozi.