KIUNGOmchezeshaji fundi wa Yanga Mnyarwanda, Haruna Niyonzima amesema kuwa hana tatizo lolote na Kocha Mkuu wa timu hiyo, Mrundi, Cedric Kaze huku akiamini ipo siku ataingia kwenye kikosi cha kwanza.

 

Mnyarwanda huyo hivi sasa amepoteza nafasi ya kudumu katika kikosi cha kwanza tangu kuanza kwa msimu huu, licha ya msimu uliopita kuwa tegemeo huku akijihakikishia nafasi ya kucheza.

 

Kiungo huyo wiki iliyopita aliongeza mkataba wa mwaka mmoja wa kuendelea kubakia kukipiga Jangwani baada ya ule wa awali kumalizika kabla ya kufikia makubaliano na uongozi na kusaini mwingine mpya.

Akizungumza na Championi Jumamosi, Niyonzima alisema kuwa, anaamini uwezo wake ndani ya uwanja, hivyo ana matumaini makubwa ya siku moja kuingia katika kikosi cha kwanza cha timu hiyo.

 

Niyonzima alisema kuwa anafurahia ushindani uliopo hivi sasa katika timu hiyo kutokana na kuwepo wachezaji wenye viwango vikubwa wanaoipa matokeo mazuri ya ushindi ambayo yamewafanya kukaa kileleni kwenye msimamo wa Ligi Kuu Bara.

Aliongeza kuwa, kikubwa hivi sasa anachoangalia ni ubingwa wa ligi pekee kwani ndiyo malengo ya wachezaji wote katika msimu ambayo wamepanga kuyatekeleza na hilo linawezekana kwao kutokana na umoja uliopo kati ya wachezaji na viongozi.“

 

Wachezaji, viongozi na mashabiki wote kitu ambacho tunakitaka ni ubingwa wa ligi pekee, kwani hayo ndiyo malengo yetu katika msimu huu tuliouanza vizuri.“

 

Hivyo kwangu najisikia faraja kuona timu inapata matokeo ya ushindi hata kama nikiwa ninaanzia benchi, ninaamini muda wangu utafika na kuanza katika kikosi cha kwanza, hakuna asiyefahamu uwezo wangu.“

 

Hivyo kurudi kwangu katika kikosi cha kwanza ni suala la muda pekee, ninafahamu mashabiki wanatamani kuniona nikirudi katika kikosi cha kwanza, niwahakikishie kuwa nitarudi kivingine,” alisema Niyonzima.

WILBERT MOLANDI,Dar es salaam