Ujerumani inatafakari kupiga marufuku ndege za abiria kutoka Uingereza na Afrika Kusini ili kuzuia kuenea kwa aina mpya ya virusi vya corona ambavyo vinaenea kwa kasi na vimethibitishwa katika mataifa hayo mawili. 

Hatua hiyo itafuata mfano wa Uholanzi na Italia, ambazo zimepiga marufuku ndege zote za abiria kutoka Uingereza kuanzia Jumapili. 

Msemaji wa wizara ya afya Ujerumani, amesema serikali inafuatilia kwa karibu hali ilivyo Uingereza na inafanya kazi katika shinikizo kubwa kutathmini tarifa mpya pamoja na data kuhusu aina hiyo mpya ya kirusi.

 Aidha ameongeza kwamba Ujerumani inawasiliana wa Ulaya kuhusu hilo. 

Ubelgiji tayari imetangaza marufuku kwa ndege zote pamoja na treni zote kutoka Uingereza. 

Wiki iliyopita, Ulaya ilikuwa bara la kwanza duniani ambalo idadi yake ya vifo kutokana na Covid-19 ilipindukia watu 500,000 tangu janga hilo lianze Disemba mwaka uliopita. 

Jumla ya watu milioni 1.6 duniani wamefariki kutokana na janga hilo na zaidi ya watu milioni 76 wameambukizwa.

 

Credit:DW