Nchi tajiri duniani zimenunua kwa wingi chanjo ya COVID-19 au corona kwa ajili ya raia wao huku kukiwa na wasiwasi mkubwa kuwa watu wa nchi masikini hawatapata chanjo hiyo muhimu.


Kwa mujibu  wa taarifa ya shirika la kutetea haki za binadamu la Amnesty International, nchi tajiri duniani zimenunua chanjo mara tatu zaidi ya zinavyohitaji, jambo ambalo linaweza kuwakosesha chanjo mabilioni ya watu katika nchi masikini. 

Canada inaongoza kwa nchi ambazo zimeagiza chanjo kwa wingi kwani uchunguzi umebaini kuwa imeagiza chanjo mara tano zaidi ya inavyohitaji. 

Uchunguzi huo umebaini kuwa mataifa tajiri ambayo yanajumuisha asilimia 14 ya watu wote duniani yameagiza asilimia 53 ya chanjo ya COVID-19 inayoonekana kuwa bora.

Imedokezwa kuwa karibu nchi 70 masikini zaidi duniani zitaweza tu kutoa chanjo moja ya COVID-19 kwa mtu mmoja kati yaa watu 10 mwaka ujao.

Shirika la Amnesty International na mashirika mengine yakiwemo ya Frontline AIDS, Global Justice Now na Oxfam, yamezihimiza serikali na makampuni yanayotengeneza dawa kuchukua hatua za kuhakikisha kuna usawa katika usambazaji wa chanjo hiyo.