MLINZI anayelinda mjengo wa ghorofa unaoendelea kujengwa wa staa wa Bongo Fleva, Rajabu Abdul ‘Harmonize’, Sande Lusembe ameibuka na kudai kuwa, anamdai pesa msanii huyo, lakini hataki kumlipa.

 

Akizungumza na Gazeti la IJUMAA WIKIENDA, Lusembe alisema kuwa, ana muda wa miaka mitatu na nusu mpaka sasa tangu aanze kufanya kazi ya ulinzi katika mjengo huo, lakini anashangaa ghafla msanii huyo alisitisha kumlipa mshahara wake, jambo ambalo linaweza kumsababishia madhara makubwa ya kumpoteza hata mkewe ambaye anaumwa.

 

“Mimi ni mtu mzima sana, ninalinda mjengo huu kwa miaka mitatu na nusu sasa, zamani nilikuwa ninapewa pesa zangu vizuri tu, lakini ghafla Harmonize akaacha kunipa pesa zangu.

 

“Kila nikimdai ananiambia nitakupa kesho mara keshokutwa, mara mama atakuletea kwa sababu mama yake ndiye huwa anakuja kuangalia hii nyumba mara kwa mara, lakini wapi, sipewi pesa yoyote ile mpaka leo, akija hapa anakaa tu ndani ya gari lake akichati, halafu anavyoondoka ndiyo utasikia mzee shika elfu kumi hiyo, sasa hiyo elfu kumi itanisaidia nini mimi na huu uzee na nyumbani nina familia?

 

“Mpaka nimewapigia simu (waandishi) uvumilivu umenishinda, nimedai pesa zangu mpaka nimechoka, sioni hata dalili ya kupata.

 

“Juzi mke wangu alifanyiwa oparesheni ya tumbo alikuwa na uvimbe, nimeomba kupewa pesa zangu ili mke wangu apate matibabu bado ninazungushwa.

 

“Mke wangu yupo hoi kitandani, kama Harmonize asiponilipa haraka atafanya mke wangu afe, naomba mnisaidie kumtafuta huenda ninyi (waandishi) atawaelewa ili nipate haki yangu.

 

“Mpaka sasa ninamdai Harmonize shilingi laki saba na ninashindwa kuondoka hapa kwa sababu kuna vitu vya thamani ndani, vikiibiwa wakati mimi sipo, anaweza kunifunga,” alisema Lusembe.

 

Gazeti la IJUMAA WIKIENDA lilimtafuta Harmo kwa njia ya simu ili kujibu tuhuma hizo, lakini simu yake iliita kwa muda mrefu bila kupokelewa na hata alipotafutwa mmoja wa mameneja wake, Beauty Mmari ‘Mjerumani’ naye hakupokea simu hivyo jitihada za kuwapata zinaendelea.

STORI: MEMORISE RICHARD, DAR