Na Jonas Kamaleki - MAELEZO
Miaka 59 ya Uhuru na 58 ya Jamhuri ni kipindi kirefu ambacho mabadiliko makubwa yameonekana yakiwemo ya kisiasa, kiuchumi na kijamii kwa ujumla.


Wakati Tanganyika inapata mwaka 1961, wahandisi wazalendo walikuwa wawili (2), kwa sasa Tanzania ina waandisi walisajiliwa na Bodi ya Usajili ya Wakandarasi (ERB) zaidi ya 19, 164 hii ikiakisi mabadiliko maridhawa katika sekta hiyo.


Makandarasi hawa wanaifanya nchi iwe na wataalaam wanaosimamia miradi mikubwa ya maendeleo ikiwemo ule wa ufuaji wa umeme wa Bwawa la Julius Nyerere ulioko Rufiji, mkoani Pwani, Ujenzi wa Reli ya kisasa yenye viwango vya kimataifa (SGR) na miradi mikubwa ya barabara, madaraja, hospitali na majengo.


Aidha, wakati Tanganyika inapata uhuru, walikuwepo wakandarasi wazawa wawili (2), mika 59 baadae nchi hii ina wakandarasi waliosajiliwa na Bodi ya Usajili wa Wakandarasi (CRB) zaidi ya 9,350. Hii inadhihirisha kuwa nchi imepiga hatua katika eneo hilo ambalo ni jambo la kujivunia.


Ikumbukwe kuwa ili Taifa liweze kuendelea vipo vitu muhimu takriban vinne, Siasa Safi na Uongozi bora, Ardhi na watu. Watu ndio nguvukazi, ndio soko la bidhaa, hivyo nchi yenye idadi kubwa ya watu, pamoja vitu vingine ina uhakika wa nguvu kazi na soko la uhakika la ndani. Tanganyika ilipopata uhuru kulikuwepo takriban watu milioni 9 na miaka 59 baada ya uhuru, nchi hii ina zaidi ya watu milioni 55.


Maendeleo hayo yamejidhihirisha pia katika nyanja ya Elimu, Afya na Miundombinu. Wakati Tanganyika inapata uhuru barabara za lami zilikuwa kilometa 360 tu wakati hivi sasa ni zaidi ya kilometa 14,000. Kipindi hicho barabara za lami ilikuwa ni kipande cha Dar es Salaam hadi Morogoro, Tanga- Korogwe na Arusha- Moshi. 


Zaidi ya hayo Tanzania imeendelea kuwa nchi ya amani na makimbilio ya nchi jirani ambazo zimekuwa zikikumbwa na machafuko ya kisiasa na kikabila. Amani hii lazima ilindwe kwani ni mtaji wa maendeleo.


Miaka 59 ya Uhuru na 58 ya Jamhuri itumike kwa watanzania kufanya kazi kwa bidii ili kujitegemea kiuchumi sawa na Kaulimbiu ya maadhimisho ya Uhuru mwaka huu isemayo “MIAKA 59 MIAKA 58 YA JAMHURI TANZANIA YENYE UCHUMI IMARA ITAJENGWA NA WATANZANIA WENYEWE, TUFANYE KAZI KWA BIDII, UWAJIBIKAJI NA UADILIFU”.


Mwisho